TANGA JIJI KUKARABATI MITAMBO YA KUZOLEA TAKA - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Tuesday, 3 November 2026

TANGA JIJI KUKARABATI MITAMBO YA KUZOLEA TAKA

 

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Jiji la Tanga, Philemon Magesa




Burhani Yakub,Tanga,


Halmashauri ya Jiji la Tanga imeanza  kuyafanyia ukarabati magari pamoja na mitambo ya kuzolea takataka ikiwa ni mikakati ya kuliweka Jiji katika hali ya usafi pamoja na kujiandaa ya ujio wa Elnino.


Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Jiji la Tanga, Philemon Magesa alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari  kuhusiana na  utekelezaji wa maagizo ya  Katibu wa Itikadi na uenezi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Kenan Kihongosi aliyotoa mwezi uliopita.


Akiwa katika ziara mkoani  Tanga, Kihongosi alieleza kusikitishwa kwake baada ya kuliona Jiji la Tanga likiwa chafu na akaagiza liwekwe katika hali ya usafi.


Magesa ambaye katika uteuzi wa hivi karibuni alihamishiwa kuwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Tanga amesema katika kuliweka Jiji hilo kuwa safi hakuna njia ya mkato ni lazima magari ya kusomba takataka pamoja na mitambo mibovu iliyopo katika dambo ifanyiwe ukarabati.


"Tayari mchakato wa kuyatengeza magari ya takataka ikiwa ni pamoja na kununua vipuri,matairi ya magari yote mabovu umeanza....tunataka kuhakikisha takataka zote zinasombwa na kupelekwa dampo Ili Jiji lirejee katika hali yake ya usafi"amesema Magesa.


Mkurugenzi huyo amesema mbali ya wafanyakazi wa Halmashauri, Jiji hilo litawatumia wadau kutoka sekta binafsi kuhakikisha mji unakuwa katika hali ya usafi ikiwa ni pamoja na kuzibua mifereji ili mvua zinazotarajiwa kunyesha zisiathiri makazi kwa kujaa maji


      MWISHO



No comments: