WASHIRIKI ZAIDI YA 3,000 KUTOKA NCHI 40 KUKUTANA ARUSHA - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Saturday, 7 November 2026

WASHIRIKI ZAIDI YA 3,000 KUTOKA NCHI 40 KUKUTANA ARUSHA

 


Na Queen Lema,Arusha


Zaidi ya washiriki 3,000 kutoka nchi zaidi ya 40 duniani wanatarajiwa kukutana jijini Arusha katika Jukwaa la Kimataifa la Biashara na Uwekezaji wa Mazao ya Bustani (HortiLogistica Africa 2026), litakalofanyika Novemba 8 hadi 10 mwaka huu katika viwanja vya TGT, likilenga kufungua fursa za biashara, uwekezaji na upatikanaji wa masoko ya kimataifa kwa wakulima wa Tanzania.


Mkuu wa Mkoa wa Arusha, CPA Amos Gabriel Makalla, amesema jukwaa hilo ni fursa muhimu kwa mkoa huo kukuza uchumi kupitia biashara na uwekezaji, huku likiimarisha nafasi ya Arusha kama kitovu cha mikutano na matukio ya kimataifa.


Akizungumza na waandishi wa habari Novemba 7, 2026, katika viwanja vya TGT jijini Arusha, Makalla amesema jukwaa hilo litafunguliwa rasmi na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius John Ndejembi, ambaye atakuwa mgeni rasmi.


Amesema jukwaa hilo linatarajiwa kuwa na waoneshaji zaidi ya 150 kutoka Afrika, Ulaya na Asia, watakaopata fursa ya kuonesha bidhaa, huduma na teknolojia mbalimbali zinazohusiana na sekta ya kilimo cha bustani.


Makalla amesema mbali na kukuza biashara ya matunda, mboga, viungo na maua, jukwaa hilo litachochea shughuli za uwekezaji katika sekta za hoteli, usafirishaji na utalii, kutokana na idadi kubwa ya wageni wanaotarajiwa kufika jijini Arusha.


Amewataka wananchi na wafanyabiashara kutumia fursa hiyo kujitangaza, kutoa huduma bora, kujenga mahusiano ya kibiashara na kunufaika na uwepo wa wawekezaji na washiriki kutoka mataifa mbalimbali, huku akiwahakikishia washiriki usalama wakati wote wa tukio hilo.

Afisa Mtendaji Mkuu wa Chama cha Wakulima wa Kilimo cha Bustani Tanzania (TAHA), Dkt. Jackline Mkindi

Kwa upande wake, Afisa Mtendaji Mkuu wa Chama cha Wakulima wa Kilimo cha Bustani Tanzania (TAHA), Dkt. Jackline Mkindi, amesema lengo la jukwaa hilo ni kuwaunganisha wakulima na masoko ya kimataifa, teknolojia za kisasa, wawekezaji pamoja na watoa huduma za usafirishaji.


Amesema kupitia jukwaa hilo wakulima watapata fursa ya kujifunza mbinu mpya za uzalishaji, kukutana na wanunuzi wa mazao yao na kupata fursa za ushirikiano zitakazosaidia kuongeza thamani na ushindani wa mazao ya Tanzania katika masoko ya kimataifa.

No comments: