Na Lilian Kasenene, Morogoro
Maipacarusha20@gmail.com
WAZIRI MKUU, Dkt. Lameck Mwigulu Nchemba, amesema vyombo vya habari imara ni rasilimali muhimu kwa Taifa na si mzigo, akisisitiza kuwa Serikali itaendelea kuviamini na kushirikiana navyo katika kuijenga jamii.
Akifungua Mkutano Mkuu wa Tisa wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Dkt. Nchemba amesema uwekezaji katika vyombo vya habari ni sehemu ya uwekezaji katika maendeleo ya jamii nzima.
"Serikali inathamini sana kazi ya vyombo vya habari na itaendelea kushirikiana navyo katika kutoa elimu kwa jamii," alisema Dkt. Nchemba.
Amesema Serikali itaendelea kutambua na kuheshimu mchango wa waandishi wa habari katika kujenga uchumi imara na jumuishi.
Aidha, Dkt. Nchemba amesema Serikali inaunga mkono juhudi za kuwawezesha vyombo vya habari kutokana na mchango wake katika ukusanyaji wa kodi, kuimarisha utawala wa sheria na kuelimisha jamii.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa TEF, Deodatus Balile, ameiomba Serikali kutoa mkopo wa shilingi bilioni 10 kwa ajili ya kusaidia uandaaji wa mitaala ya kisasa ya uandishi wa habari.
"Mitaala na ujuzi unaotumiwa na waandishi wa habari umepitwa na wakati. Tunahitaji mikopo ili kuandaa mitaala itakayowawezesha waandishi wa habari kwenda sambamba na mabadiliko ya kitaaluma," alisema Balile.
Balile ameongeza kuwa elimu zaidi inahitajika katika tasnia ya habari, hususan kwa vijana wanaoingia na kufanya kazi katika sekta hiyo.
Amesema ni muhimu kutumia uzoefu na maarifa ya wanahabari wastaafu na wakongwe kuwajengea uwezo vijana ili waweze kukabiliana na mabadiliko ya tasnia ya habari.
Katika mkutano huo pia ulifanyika uchaguzi wa kujaza nafasi ya Makamu Mwenyekiti wa TEF, ambapo Joyce Shebe aliibuka mshindi dhidi ya mgombea mwenzake, Salome Kitomari.
Nafasi hiyo ilikuwa ikishikiliwa na Bahari Machimu, ambaye kwa sasa amepangiwa majukumu mengine na Serikali.
.......

No comments:
Post a Comment