ASASI ZA KIRAIA ZASHAURI NJIA BORA ZA KUTATUA MGOGORO WA ARDHI NGORNGORO - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Monday, 21 March 2022

ASASI ZA KIRAIA ZASHAURI NJIA BORA ZA KUTATUA MGOGORO WA ARDHI NGORNGORO

MGOGORO wa Ngorongoro umechukua sura mpya baada ya Mashirika 20 ya kutetea  haki za wafugaji wa asili kutoa tamko wakilaani udhalilishwaji unaofanywa na watu wenye nia mbaya wakiwemo wanasiasa na baadhi vyombo vya habari dhidi ya wakazi wa eneo hilo.

Aidha wamelaani jaribio lolote la kukiuka haki za binadamu katika sakata hilo huku wakizitaka pande zote zinazohusika na mgogoro huo zijielekeze kwenye kujibu hoja na sio kushambuliana kwa maneno makali.



Wameyasema hayo Machi 18,2022  kwenye mkutano na waandishi wa habari uliofanyika jijini Arusha ambapo tamko hilo limesomwa na Mkurugenzi wa mtandao wa wafugaji nchini, Joseph Parsambei, Afisa Mipango wa MPDO, Amani Sekino na Msaidizi wa kisheria wa EPO Karatu, Agness Marmo kwa niaba ya wenzao waliokuwa pamoja nao.

Wamesema wanashauri itumike meza ya majadiliano katika kupata suluhisho la kudumu la mgogoro huo huku wakitaka kuwe na ushirikishwaji wa mashirika ya kiraia katika mchakato huo ili nao waweze kutoa ushauri wao kwani nao ni sehemu ya jamii.

 


“Tumeendelea kushuhudia matamko mbalimbali na vita ya maneno kati ya baadhi ya watu wakiwemo wabunge, Waziri wa Maliasili na utalii na viongozi wa jamii. Tunataka kila upande uheshimu sheria za nchi, haki za binadamu na utawala bora,” amesema Parsambei akisoma tamko hilo.

Tamko hili limekuja siku nane  baada ya Waziri Mkuu, Majaliwa Kasim Majaliwa kukutana na viongozi wa kimila jamii ya kimaasai, Malaigwanak jijini Arusha na kukabidhiwa na mkuu wa mkoa wa Arusha, John Mongela jumla ya majina ya kaya 86 zenye watu  453 ambao kwa hiari yao wamekubali kuhama kwenye eneo la Hifadhi ya Ngorongoro.

 

Taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu ilidai kuwa hayo ni matokeo ya vikao  vya kiongozi huyo na wadau wa uhifadhi vilivyofanyika Februari 14 na 17, mwaka huu kwenye tarafa za Loliondo na Ngorongoro Wilayani Manyara. 

Siku mbili baadaye Majaliwa alienda kukagua mradi wa ujenzi wa nyumba mpya 103 kwenye kijiji cha Msomera wilayani Handeni mkoani Tanga ambazo ni maalum kwa ajili ya wale wanaohama kwa hiari kutoka kwenye eneo la hifadhi ya Ngorongoro.

Alisema kuwa kwenye hatua hiyo ya kwanza serikali imetenga kiasi cha shilingi bilioni 1.2 ambapo serikali imeshapima viwanja 2,500 na kutenga eneo la ekeri 1,700 kwa ajili ya kilimo na malisho huku akisisitiza kuwa serikali itahakikisha haki za binadamu zinazingatiwa katika zoezi hilo.



Akisoma tamko la asasi hizo, Marmo amesema  kuwa eneo la tarafa ya Ngorongoro lina ukubwa wa kilometa za mraba 8,000 ambapo mgogoro ni kati ya serikali na wananchi kwa madai ya ongezeko la watu na mifugo.

Tarafa ya Loliondo ina ukubwa wa kilometa za mraba 4,000 ambapo eneo la mgogoro ni kiliometa za mraba 1,500 ya ardhi ya vijiji iliyopo tarafa hiyo pamoja na Sale huku mgogoro ukihusisha Serikali, Wawekezaji na wananchi.

Marmo amesema kuwa eneo la tarafa za Loliondo na Sale linatumika na wananchi kwa ajili ya shughuli zao ikiwemo makazi na ufugaji na yamesajiliwa kwa mujibu wa sheria ya uanzishwaji vijiji ya mwaka 1978 hivyo wapo hapo kilali.

 

“Eneo hilo lina kesi mahakamani hivyo uhuru wa mahakama uheshimiwe na upotoshwaji unaofanywa na watu wenye maslahi mbalimbali dhidi ya jamii ya wafugaji ukome mara moja,” amesema Marmo bila kuwataja watu hao na kuongeza.

 … Tunaomba Serikali na jamii wakae kwenye meza huru ya majadiliano na wakubaliane namna ya matumizi ya eneo hilo. Sisi asasi za kiraia tunaendelea kuwa macho na kufuatilia kwa ukaribu sakata hili.

 

Marmo amesema kuwa matumizi endelevu ya ardhi ni suluhisho la mgogoro kwenye eneo hilo hivyo akashauri wadau wote wajikite katika mrengo huo ili maslahi ya wote yaweze kulindwa.

 

“Serikali pamoja na wadau wengine wa maendeleo wawezeshe matumizi endelevu ya ardhi ili kutoa suluhu ya kudumu ya mgogoro huu,” alisisitiza Marmo.

 


Kwa upande wake Sekino amesema kuwa eneo la tarafa ya Ngorongoro lina umuhimu wake na sheria maalum inayosimamia matumizi yake jambo walilodai kuwa endapo sheria hiyo ikitumiwa vizuri inaweza kuwa nyenzo ya kutatua mgogoro huo bila kuathiri maslahi ya upande wowote.

 

“Ngorongoro ni nyumbani kwa wafugaji na ni eneo la matumizi mseto hili ni muhimu sana lifahamike na kuheshimiwa. Utatuzi wa mgogoro huu ni meza huru ya mazungumzo kati ya pande zote mbili,” alisema Sekino.



Asasi za kiraia zilizosaini tamko hilo ni pamoja na TPCF, Equity Paralegal Organization, Leshaabingo, Lareto le sheria, Oseremi, Ngorongoro Paralegal Foundation, Sauti Zetu Paralegals Organizatio, PALSEF na ALAPA.

 

Nyingine ni Embuan Development Organization, CILAO, MPDO, Media Aid Indigenous and Pastoralist Community, (MAIPAC), Tanzania Pastoralist and Hunter-Gathers Organization, ( TAPHGO), Media Defense Initiative, (MDI), Ngorongoro Education Development Organization, (NEDO), Tanzania Centre for Research and Information on Pastoralist, (TCRIP), Indigenous Heartland Organization, (IHO), Mimutie Womea Organization, (MUMETI) na  Intergral Development Initiative in Ngorongoro,(IDINGO).

No comments: