MAIPAC TEAM, Monduli.
Hifadhi ya Jamii ya wanyamapori(WMA) ya Randilen iliyopo wilaya ya Monduli, mkoa wa Arusha, imepewa msaada wa gari aina ya Landcrusser ambalo linatumia umeme wa jua katika mawasiliano ili kufanya doria za kukabiliana na majangili.
Msaada huo, umetolewa na Taasisi ya uhifadhi ya The Nature Conservancy, ikiwa ni sehemu ya miradi yake ya uhifadhi na nyanda za malisho katika maeneo ya WMA hapa nchini.
Akikabidhi gari hilo hivi karibuni, Mkuu wa wilaya ya Monduli, Frank Mwaisumbe aliwataka viongozi wa WMA ya Randilen kuitumia gari hilo kwa malengo yaliyokusudiwa.
Mwaisumbe alisema msaada huo wa utasaidia sana kuimarisha doria katika hifadhihiyo ambayo inapakana na hifadhi ya Taifa ya Tarangire.
"Tunapongeza The Nature Conservancy kwa msaada huu kwani umekuja wakati muafaka ambapo Rais Samia Suluhu amefungua fursa za utalii nchini na kuvutia mamilion ya watalii duniani kuja Tanzania"alisema
Awali Mkurugenzi wa taasisi ya The Nature Conservancy (TNC),Alphonce Mallya alisema gari hilo limegharimu kiasi cha sh 127 milioni na limefungwa mifumo ya umeme wa jua ili kusaidia mawasiliano wakati wote.
Mallya alisema gari hilo ni sehemu ya misaada ambayo imekuwa ikitolewa kwa WMA ili kuimarisha utendaji wake katika kuendeleza hifadhi hiyo ambayo ni kivutio cha watalii kwa sasa.
Afisa miradi wa taasisi hiyo, Warda Kanangwa alisema gari hilo litatumika kutoa huduma za doria na kudhibiti wanyama waharibifu katika vijiji vinane vinavyoundwa WMA hiyo.
Kanangwa alitaja vijiji hivyo kuwa ni Swakini juu, Oldonyo,Naitolia,Mswakini, Lemoti,Lengorwa,Loksale na kijiji cha Nafco.
Meneja wa Randileni WMA Meshurie Melembuki alisema msaada huo utapunguza uhaba wa magari katika hifadhi hiyo kwani, walikuwa na mahitaji ya magari manne na sasa wamepata mawili.
"bado tunahitaji gari moja kwani eneo letu lahifaadhi lenye kilomita za mraba 312 ni kubwa kufanya doria wakati wote na awali walikuwa na garimoja pekee"alisema
Hata hivyo, Melembuki alishukuru taasisi hiyo kuendelea kuwasaidia miradi mbali mbali na akatumia fursa hiyokualika watalii wa ndani na nje ya nchi kutembelea hifadhi hiyo.

No comments:
Post a Comment