Mwandishi wetu, Maipac
maipacarusha20@gmail.com
Arusha.Nchi wanachama wa Umoja wa Afrika(AU) zimeombwa kutekeleza hukumu zinazoatolewa na Mahakama ya Afrika ya Haki za Binaadamu na Watu(AFCHPR) Ili kuendeleza misingi ya Haki za binaadamu katika nchi wanachama.
Mahakama hiyo ilianzishwa mwaka 2004 kutokana na maazimio ya Umoja wa Afrika ya mwaka 1998, Makao makuu yake yapo jijini Arusha,hata hivyo, imekuwa na changamoto ya nchi kadhaa wanachama wa umoja wa Afrika(AU) kutotekeleza hukumu ambazo zimekuwa zikitolewa.
Rais wa mahakama hiyo, Jaji Imani Aboud akizungumza katika ufunguzi wa mwaka wa mahakama hiyo Leo February 20,2023 jijini Arusha , amesema bado nchi nyingi katika hazitekelezi hukumu za Mahakama hiyo .
Amesema mahakama hiyo ipo kisheria na imeundwa na AU na kwa mujibu wa mkataba wa AU ibara ya 30 nchi wanachama zinapaswa kuheshimu maamuzi ya mahakama hiyo.
Jaji Iman amesema tangu mahakama hiyo ilipoanzishwa miaka 16 iliyopita imeweza kutoa hukumu katika mashauri zaidi ya 200 ambayo yalifikishwa kutoka nchi mbalimbali
" changamoto iliyopo ni baadhi ya nchi kutotekeleza baadhi ya hukumu ambazo zimekuwa zikitolewa na mahakama hii "amesema
Akizungumza katika hotuba ya ufunguzi wa mwaka wa mahakama hiyo, 2023 Makamu wa Rais wa Jamuhuri ya Muungano Dk Philip Mpango amesema, Serikali ya Tanzania inatambua umuhimu wa mahakama hiyo na itaendelea kufanya nayo kazi .
Hata hivyo, amesema kumekuwepo na changamoto kadhaa katika utekelezwaji wa hukumu za mahakama hiyo na akashauri mahakama kuboresha mahusiano na mahakama za ndani ya nchi, ili kuondoa dhana kuwa mahakama hiyo kuingilia uhuru wa mahakama za ndani.
Amesema ni muhimu kuwepo na ushirikiano na mafunzo baina ya watendaji wa mahakama majaji, Mawakili na mahakimu juu ya masuala ya haki za binaadamu .
Kauli mbiu ya mwaka wa mahakama hiyo mwaka huu ni "kuunganisha mifumo wa sheria za haki za binaadamu za kikanda na kimataifa katika mifumo ya kitaifa"
Awali Rais wa mahakama ya Afrika ya Mashariki Jaji Nestor Kayobera na Rais wa bunge la Afrika, Fortune Charumbira walieleza kuridhishwa na kazi nzuri ambayo inaendelea kufanya na mahakama hiyo katika kulinda na kutetea na haki za binaadamu barani Afrika.
Katika ufunguzi wa shughuli za Mahakama hiyo,pia wamehudhuria majaji wa mahakama za ndani ya nje,majaji wa mahakama ya Afrika ya Mashariki, Mawakili, wawakilishi wa mashirika ya kutetea haki za binaadamu na viongozi wa Serikali ngazi mbalimbali akiwepo Waziri wa Katiba na Sheria Dk Damas Ndumbaro.
No comments:
Post a Comment