SHUHUDIA HAPA MCHANGA WA MAAJABU UNAOTEMBEA HIFADHI YA NGORONGORO, UNATUMIKA PIA KUSAKA MIMBA KWA WANAWAKE - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Sunday 26 February 2023

SHUHUDIA HAPA MCHANGA WA MAAJABU UNAOTEMBEA HIFADHI YA NGORONGORO, UNATUMIKA PIA KUSAKA MIMBA KWA WANAWAKE

Mchanga unaotembea wa Ngorongoro Moja ya sehemu inayovutia watalii wengi katika hifadhi ya Ngorongoro.



Mwandishi wetu, Maipac 

maipacarusha20@gmail.com


Ngorongoro.Watalii na watafiti kutoka maeneo mbali mbali duniani, wanatarajiwa kuongezeka ndani ya eneo la Mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro, kushuhudia mchanga unaotembea ambao sasa kuna taarifa za awali za kitafiti zinaeleza unafanana na mchanga uliopo katika sayari ya Mars.


Mataifa makubwa duniani, ikiwepo Marekani na China, yamekuwa yakiendelea na tafiti mbali mbali katika sayari ya Mars ikiwepo kutazama kama kuna uwezekano wa ardhi  iliyopo katika sayari hiyo,kutumika na binaadamu.


Kamishna msaidizi mwandamizi wa uhifadhi, Joshua Mwamkunda,  anasema utafiti unaendelea kubaini aina ya mchanga huo unafanana kiasi gani na mchanga uliopo sayari ya Mars.


"hizi ni taarifa za awali bado tafiti zitaendelea juu ya mchanga huu ya ajabu ambao unatembea wastani wa  mita 17 kwa mwaka  ikiwa sawa na sentimita  4.7 kwa siku"anasema

Anasema mchanga huo ni sehemu ya vivutio vya kijiolojia  ambavyo vinapatikana katika eneo la Mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro. 

Godfrey Ole Moita mhifadhi wa mambo kale, katika eneo la Mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro, anasema tafiti zaidi zimekuwa zikiendelea  katika mchanga huo na  bonde lote la Olduvai ambapo kumebainika mabaki na masalia za zamadamu,wanyama na visukuku.

Anasema awali mchanga huo, ulibainika umetokana na mlipuko wa volcano wa mlima odonyolengai ulipo jirani na eneo hilo .

Anasema mchanga huo pia unatumiwa na jamii ya kimasai kwa shughuli za kitamaduni ikiwepo ama  kutafuta mtoto kwa wanafamilia ambao wamekuwa na tatizo la kupata ujauzito.


Tafiti zinaonesha mchanga huu, ulitupwa miaka mingi iliyopita  ingawa kwa mara ya mwisho,Mlima huu, ulilipuka kwa mshindo mkubwa  kati ya mwaka 1964 na 1966.

Mchanga, huu unatembelea kuelekea eneo la mashariki la Mlima Oldonyo Lengai ukiwa na urefu wa mita tano na upana na mita 100 na kutengeneza umbo kama mwezi mchanga.


Maria Sabore,anaelezea maajabu ya mchanga    wanauheshimu sana kama mchanga wa kutoka  mlima Oldonyo lengai (Mlima wa Mungu).

Sabore anasema, tangu yeye amezaliwa amekuta mchanga  huo, ukiwa na heshma kubwa sana kwa jamii yao.

Anasema mchanga umekuwa ukisaidia kupunguza matatizo ya kifamilia mengi kama kushindwa kupata mtoto, ugomvi ndani ya familia na pia kuomba msamaha kwa mungu.

Anasema kutosambaa kwa mchango huo, tangu kuanza safari yake na kuwa na kitu kama sumaku ya kuwaunganisha kunawafanya waamini huo ni mchanga wa Mungu.


    Jinsi ya kusaka Mimba kwa mchanga.


Sabore anasema wamekuwa na utaratibu wa kwenda katika mlima huo, kusaidia akina mama na wasichana kupata mimba.

Anasema  unapaswa kujiandaa, kutafuta boma(familia ambayo haina migogo na inaheshima katika jamii ya kimasai.

Sabore anasema katika familia hiyo, ambaye unatafutra mtoto, utatakiwa kupata wasichana wanne ambao, hawajazaa na hawajawahi kushiriki tendo la Ndoa.
 

Anasema pia utatafuta wazee wanne wa heshma ambao hawana historia ya ukorofi au kufanya mambo mabaya katika jamii yao.

Sabore anasema , utapaswa kutafuta Kondoo mmoja mzuri na mtaandamana wote kwenda kwenye mchanga, nnaweza kusindikizwa na wanawake wengine.

Anasema ila wasichana wanne, wao ndio watakuwa wamemshika Kondoo na  akina mama wengine watakuwa  vibuyu vya maziwa na majani ya kijani kuonesha amani na upendo kuelekea kwenye  mchanga.

Sabore anasema ukifika, eneo la mchanga basi, wale wazee wanne, watamchinja Kondoo na kumwaga damu juu ya mchanga na  akina mama wataweka maziwa kwenye mchanga.

Anasema wazee hawa, baadaye watatembea kuelekea upande wa mashariki,kuzunguka mchanga mara nne wakiwa wanamuomba mungu amalize tatizo lako huku akina mama wakiimba na kucheza kwa furaha na kumuomba pia mungu.

Baadaye yale majani yatawekwa juu ya mchanga na sehemu ya maziwa na wenye zawadi nyingine kama shanga, mikanda na bangili wataweka kama ishara ya kutoa sadaka kwa mungu.

Anasema baada ya tukio, hilo akina mama hao na wazee, watarudi kwenye boma moja lililoteuliwa  na hapo nyama ndio itagawanywa na wazee hao na watu kula.

Maria Babore na Mwenzake Malasia Nengoyo na Elizabeth Mondelele wakiwa katika moja ya maboma ya kimasai wakielezea mchanga huu na maajabu yake.


“baada ya tukio hilo zoezi la kusaka mimba litakuwa limekamilika na hapo  mwanamke au msichana ambaye anasaka Mimba atarejea kwa mumewe na muda si mrefu mimba itakuwa imetunga”anasema                  

Huu ndio mchanga wa ajabu wa Ngorongoro ambao unanguvu za ajabu za kusaidia kupatikana mimba na pia kumaliza matatizo mengine baada ya kumuomba mungu ukiwa umesimama juu yake na kuwa na Imani.

Mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro ni moja ya maeneo ya kipekee duniani, ambayo yanakabiliwa na maajabu lukuki.

Maajabu ya Ngorongoro, yamelifanya eneo hilo, kuwa ni moja ya maeneo yaliyoteuliwa kuwa ni maeneo ya  urithi wa dunia ambayo yanalindwa kimataifa na shirika la umoja wa mataifa ya elimu , Sayansi na Utamaduni(UNESCO) lakini pia moja ya maeneo ya utalii wa kiikolojia barani Afrika.

Ngorongoro pia kutokana na maajabu yake, ambayo ni kivutio kikubwa cha utalii, yamelifanya eneo hili, kushinda tuzo ya moja kati ya maeneo saba ya kuvutia ya asili barani Afrika.

Katika eneo hili la Ngorongoro ndipo kumegundulika Nyayo za zamadamu wa kale walioishi miaka milioni 3.6 , nyayo ambazo zinawavutia wanasayansi wa kale kuanza kuhisi mwanadamu wa kwanza aliishi ukanda ya Ngorongoro.

Ngorongoro pia kuna maajabu ya kuwa na creta, ambapo wanyama wa aina nyingi, wakiwepo Simba, Faru, Nyati,Viboko na wengine lukuki wanaishi pamoja.

No comments: