Kamanda wa Polisi Mkoani Arusha Justine Masejo akizungumza na wanaahabari |
NA: Mwandishi wetu, MAIPAC Arusha
maipacarusha20@gmail.com
JESHI la Polisi Mkoani Arusha limewafukuza kazi askari wake sita katika kipindi cha miezi sita, kutokana na makosa mbalimbali ya utovu wa nidhamu yasiyoendana na maadili ya jeshi hilo.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana,bila kuwataja majina ya askari hao, Kamanda wa polisi mkoani hapa, Justine Masejo alisema kuwa askari hao walifukuzwa kazi katika kipindi hicho baada ya uchunguzi wa kijeshi kukamilika kutokana na makosa yaliyokuwa yakiwakabili.
Alisema kuwa utaratibu wa kuchukuliana hatua za kinidhamu ndani ya jeshi la polisi ni jambo la kawaida hasa kwa askari wanapokiuka maadili ya jeshi hilo.
"Katika kipindi cha miezi sita tumewafukuza askari wetu sita wakikabiliwa na makosa mbalimbali ya utovu wa nidhamu,kama mnavyojua askari wetu wanaoajiriwa wanatoka kwenye jamii ,hivyo matukio ya utovu wa nidhamu lazima yawepo"
Wakati huo huo, kamanda Masejo alisema kuwa katika kipindi cha mwaka jana 2022,watu wapatao 241 walihukumiwa na kufungwa jela baada ya kufikishwa mahakamani kutokana na makosa ya ubakaji na ulawiti.
Alisema matukio ya ubakaji na ulawiti yamekuwa yakiongezeka ingawa jeshi hilo limekuwa likitoa elimu kwa jamii kupitia vipindi vya Radio.
Katika tukio jingine Kamanda Masejo amesema kuwa jeshi la polisi limefanikiwa kumtia mbaroni mwanaume mmoja mwenye miaka 46 mkazi wa Sombetini jijini Arusha,akituhumiwa kumlawiti mtoto wake wa kumzaa anayesoma darasa la Kwanza.
Katika tukio jingine mahakama ya hakimu mkazi jijini Arusha imemkuta na hatia,Kelvin Wilfred (19) mkazi wa Muriet na kumhukumu kifungo cha Maisha jela kwa kosa la kumbaka mwanafunzi wa darasa la nne.
Wakati huo huo mahakama za wilaya ya Karatu,Monduli na Arumeru zimewahukumu kifungo cha Maisha watu wanne na wengine wanne wakihukumiwa kifungo cha miaka 30 jela baada ya kuwakuta na hatia katika makosa ya ubakaji na ulawiti.
Kamanda Masejo aliwataja waliohukumiwa kifungo cha Maisha kwa makosa ya ulawiti ni,Peter Leonard (27)mkazi wa Lashaine ,Monduli,Paulo Hilonga(60) mkazi wa Karatu ,John Sanare mkazi wa Arumeru na Elias Ndosikoi mkazi wa Arumeru.
Alisema wengine waliohukumiwa kifungo cha miaka 30 kwa makosa ya ubakaji ni James Elirehema,Elias Robert (27), Japhet Mungure wote wakati wa Arumeru pamoja nanTheophili Salaho (32) mkazi wa Karatu
No comments:
Post a Comment