RIDHIWANI KIKWETE ATAKA SULUHU MIGOGORO YA ARDHI WAKAZI WA CHAMAKWEZA - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Monday 20 February 2023

RIDHIWANI KIKWETE ATAKA SULUHU MIGOGORO YA ARDHI WAKAZI WA CHAMAKWEZA

 

NAIBU Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mheshimiwa Ridhiwani Kikwete akizungumza na wakazi wa Chamakweza

NAIBU Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mheshimiwa Ridhiwani Kikwete akisalimiana na wakazi wa Chamakweza

NA:JULIETH MKIRERI, MAIPAC CHALINZE
 
maipacarusha20@gmail.com

NAIBU Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mheshimiwa Ridhiwani Kikwete  ametoa maagizo kwa wakazi wa Kijiji cha Chamakweza Kata ya Vigwaza kukaa pamoja na kutatua migogoro yao kabla hatua nyingine hazijachukuliwa.

Kikwete ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Chalinze alitoa maagizo hayo juzi alipokutana na wananchi hao katika ziara yake ya kusikiliza kero za wananchi ambapo katika kijiji hicho upo mgogoro wa muda mrefu kati ya wakulima na wafugaji.

Akizungumza katika mkutano huo amesema Chamakweza kumekuwa na mambo ambayo hayaendi sawa kwa muda mrefu kati ya jamii mbili za wakulima na wafugaji hali inayochangia baadhi ya mipango ya maendeleo kushindwa kufanyika kama ilivyopangwa.

" Wazee kaeni tafuteni suluhu ya migogoro mliyo nayo kama mmeshindwa kutafuta amani yenu wenyewe niambieni nitawaonyesha inavyopatikana, nitarudi hapa Machi katikati nikute matatizo yamemalizika tujadili mengine" amesema.

Kikwete amesema wananchi hao kabla ya kuikaribisha serikali kuingilia migogoro yao wanatakiwa kuitatua wenyewe kwa kufanya vikao vitakavyowahusisha wazee katika kutafuta suluhu.

Amesema mgogoro wa mpaka uliopo kati ya  Chamakweza na Pingo hauwezi kutatuliwa iwapo wenyeji wa Chamakweza wenyewe kwa wenyewe hawaelewani kwa kila mmoja kusimamia uhalali wake wa kuishi katika eneo hilo huku kukiwa na migongano ya kila siku inayokwamisha maendeleo.

Katika hatua nyingine Kikwete amesema Serikali imebaini uwepo wa migogoro mingi ya ardhi na hivyo inatarajia kupima na kutoa hati miliki za ardhi katika mikoa yote hapa nchini.

Kwa mujibu wa Kikwete katika utekelezaji huo Serikali imetenga zaidi ya Bilioni 300 lengo likiwa ni kuondoa migogoro ya ardhi iliyokithiri katika maeneo mbalimbali ambayo imekuwa kikwazo cha kufikia malengo ya maendeleo yanayopangwa.

Awali akizungumza katika mkutano huo Diwani wa Vigwaza Mussa Gama amesema kijiji cha Vigwaza kinakabiliwa na vikwazo vya maji na mgogoro wa mpaka.

No comments: