RIDHIWANI KIKWETE AZITAKA SERIKALI ZA VIJIJI KUORODHESHA WAWEKEZAJI WASIOENDELEZA MIRADI YAO - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Thursday 23 February 2023

RIDHIWANI KIKWETE AZITAKA SERIKALI ZA VIJIJI KUORODHESHA WAWEKEZAJI WASIOENDELEZA MIRADI YAO

 

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Ridhiwani Kikwete akizungumza na wakazi wa Kata ya Lugoba

NA: JULIETH MKIRERI, MAIPAC CHALINZE 



NAIBU Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Ridhiwani Kikwete amezitaka Serikali za Vijiji kuorodhesha majina ya wawekezaji ambao wamehodhi ardhi bila kuiendeleza ili irudishwe kwa ajili ya matumizi mengine.

Ameyasema hayo alipokuwa kwenye ziara Kata ya Lugoba Halmashauri ya Chalinze kuzungumza na wananchi kutatua kero na changamoto kwenye Jimbo la Chalinze ambapo yeye ndiyo Mbunge wa Jimbo hilo.

Kikwete amesema kuwa maeneo mengi aliyopita kikiwemo Kijiji cha Makombe  kumekuwa na malalamiko mengi toka kwa wananchi juu ya baadhi ya maeneo yaliyoombwa na wawekezaji hayajaendelezwa na kuwa mapori.

"Vijiji na Vitongoji orodhesheni majina ya wawekezaji wote walio katika maeneo yenu ambao hawajaendeleza ardhi waliyoiomba kufanya uwekezaji lakini wameiacha bila kuiendeleza kwani huo siyo utaratibu ni vema wakanyanganywa na kupewa watu wengine ili kuyatumia kuleta maendeleo,"amesema 

Naye Diwani wa Lugoba Rehema Mwene amesema kuwa Kijiji cha Makombe kinakabiliwa na changamoto ya ubovu wa barabara, ukosefu wa maji, uchakavu wa Zahanati na baadhi ya maeneo kukosa umeme.

Mwene amesema kuwa changamoto nyingine ni baadhi ya wawekezaji kuchukua maeneo na kutoyaendeleza hivyo kufanya kuwe na mapori makubwa ambayo yanahatarisha usalama wa watu.

Kwa upande wake kaimu Mtendaji wa Kijiji cha Makombe Godfrey Nyange akisoma risala ya Kijiji amesema kuna migogoro ya mipaka baina ya Kijiji hicho na Vijiji vya Kinzagu na Mindutulieni.

No comments: