TANZANIA NA ANGOLA ZASAINI HATI ZA MAKUBALIANO - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Thursday 16 February 2023

TANZANIA NA ANGOLA ZASAINI HATI ZA MAKUBALIANO

 







NA: Mwandishi wetu

maipacarusha20@gmail.com

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Jamhuri ya Angola zimesaini Hati mbili za Makubaliano (MoUs) za kuanzisha Tume ya Kudumu ya Pamoja (JPC) na Hati ya Ushirikiano kati ya Chuo Cha Diplomasia cha Tanzania (CFR) na Chuo cha Venancio de Moura cha Angola.

 

Makubaliano hayo yamesainiwa leo na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax (Mb.) na Waziri wa Mambo ya Nje wa Angola, Mhe. Balozi Téte António katika Ofisi za Ubalozi wa Tanzania, Addis Ababa nchini Ethiopia.

 

Mara baada ya kusaini kwa Hati hizo za Makubaliano, Dkt. Tax alisema Tanzania na Angola zimekuwa zikishirikiana kwa muda mrefu, na Tanzania ilikuwa mstari wa mbele kuzisaidia nchi za kusini mwa Bara la Afrika kujikomboa na tangu wakati huo imeendelea kushirikiana katika maeneo mbalimbali.

 

“Leo tumeona ni vyema turasimishe ushirikiano wetu kwa sababu dunia inakwenda mbele na kuna mambo mengi ya kufanya pamoja na hivyo tumesaini Hati mbili za Makubaliano ya kuanzisha Tume ya Kudumu ya Pamoja itakayotuwezesha kukutana na kujadili masuala mbalimbali yenye manufaa kwa pande zote mbili.

 

………lakini sisi kwa kuwa ni wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), Umoja wa Afrika (AU) tutaweza kujadili yale yanayojiri katika Kanda zetu na Kimataifa na kuona tunaweza kuyafanyia kazi kwa namna gani kwa pamoja kwani umoja ni nguvu,” alisema Dkt. Tax

 

Kuhusu Hati ya Makubaliano ya Ushirikiano wa Vyuo vya Diplomasia kati ya Tanzania na Angola, Waziri Tax alisema kuwa kupitia makubaliano hayo vyuo hivyo vitaweza kubadilishana uzoefu, utaalamu na wanafunzi ili kuboresha zaidi taasisi zetu hizi za diplomasia.

 

“Kupitia makubaliano tuliyosaini leo, vyuo vyetu vya Dioplomasia vitaweza kubadilishana uzoefu, utaalamu na wanafunzi ili kuboresha zaidi taasisi zetu hizi za diplomasia,” alisema Waziri Tax.

 

Kwa Upande wake, Waziri wa Mambo ya Nje wa Angola, Mhe. Balozi Téte António amesema Angola imefurahishwa na uamuzi wa Serikali ya Tanzania kukubali kuanzisha Tume ya Kudumu ya Pamoja (JPC) na kuelezea utayari wake wa kushirikiana katika nyanja mbalimbali kwa maslahi ya pande zote mbili.

 

“Tanzania na Angola ni marafiki wa siku nyingi, kupiti makubaliano tuliyosaini leo tumefungu ukurasa mpya wa ushirikiano baina ya mataifa yetu, tunayo mengi ya kushirikiana. Kadhalika, kuhusu ushirikiano wa vyuo vyetu Waangola tumekuwa tukija kujifunza masuala mbalimbali ya kidiplomasia katika Chuo cha Diplomasia (CFR) na kuwa wanadiplomasia, hivyo kupitia makubaliano ya leo tutaweza kubadilishana uzoefu wa kidiplomasia pamoja na kuwanoa wanadiplomasia wengi zaidi,” alisema Balozi António. 

No comments: