Na Mwanadishi wetu, Mirerani
maipacarusha20@gmail.com
WAJUMBE
wa Baraza la Mamlaka ya Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani
Manyara, wamechangia sh20,000 kila mmoja ili kuwapongeza na kuwafanyia
sherehe walimu wa sekondari ya Mirerani B.W. Mkapa kwa kufaulisha vyema
wanafunzi wa kidato cha nne.
Wajumbe wa mamlaka hiyo wamechanga
kiasi cha sh20,000 kila mmoja ili kuwezesha sherehe ya kuwapongeza
walimu wa shule ya sekondari Mirerani B.W. Mkapa itakayofanyika mwishoni
mwa mwezi huu.
Diwani wa kata ya Endiamtu, Lucas Zacharia
akizungumza kwenye kikao cha baraza la mamlaka hiyo amesema walimu wa
shule hiyo wanapaswa kupongezwa ili kuungwa mkono.
Zacharia
amesema walimu wa shule hiyo wamejitahidi mno kuhakikisha wanafunzi
wanafanya vyema kwani hata masomo ya hesabu na sayansi yaliyozoeleka ni
magumu, wamefaulu.
“Walimu wamejitahidi mno kwani hakuna daraja
sifuri, wanafunzi 13 wamepata daraja la kwanza, wanafunzi 42 daraja la
pili, wanafunzi 61 daraja la tatu na 43 daraja la nne,” amesema.
Mwenyekiti
wa mamlaka ya mji mdogo wa Mirerani, Adam Kobelo amesema wajumbe
wameridhia kuchanga kwanza fedha zao wenyewe kisha wadau wengine nao
watafuatwa.
“Tutaunda kamati maalum ambayo itafanikisha sherehe
ya kuwapongeza walimu ili mwaka huu tena wawafundishe vyema watoto wetu
na mwakani wafaulu zaidi,” almesema Kobelo.
Diwani wa kata ya
Mirerani Salome Nelson Mnyawi amesema walimu hao wanastahili kupongezwa
kwani wameipa sifa Mirerani kutokana na ufaulu huo wa wanafunzi wa
kidato cha nne.
Amesema anatarajia walimu hao hawatabweteka ila
wataongeza juhudi katika kufundisha ili watoto wa mji wa Mirerani wapige
hatua kubwa kwenye suala la elimu na taaluma kwa ujumla.
Mjumbe
wa bodi ya shule hiyo Jema Lilama amepongeza hatua hiyo ya viongozi hao
kuandaa sherehe kwa ajili ya kuwapa mkono wa shukrani walimu wa shule
hiyo.
“Shule hii inazidi kutupa heshima kwenye mji wetu wa
Mirerani kwani watoto wetu watakuja kuwa wataalam kwenye miaka ijayo na
kusaidia jamii,” amesema Jema.
Mwenyekiti wa kitongoji cha
Tanesco, Justin Abraham amesema walimu hao wamewatoa kimasomaso wananchi
wa mji mdogo wa Mirerani kutokana na matokeo hayo ya kidato cha nne.
"Mara
ya kwanza walifanikisha mwanafunzi mmoja kuchaguliwa kwenda kidato cha
tano shule ya sekondari Tabora boys, leo wametokomeza ziro wanastahili
kupongezwa kwa kweli," amesema.
No comments:
Post a Comment