ASKARI WA WANYAMAPORI WAJENGEWA UWEZO UKAMATAJI MAJANGULI, UPELELEZI NA UPEKUZI - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Wednesday 15 March 2023

ASKARI WA WANYAMAPORI WAJENGEWA UWEZO UKAMATAJI MAJANGULI, UPELELEZI NA UPEKUZI

Mwendesha Mashitaka wa TAWA Getrude Kariongo akitoa mafunzo kwa askari wa wanyamapori

 
Mwanasheria kutoka ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka mkoa Manyara Brandina Msawa akitoa mafunzo kwa askari wa wanyamapori

Askari Wanyamapori wa Burunge WMA, Askari wa taasisi ya Chemchem na kutoka halmashauri ya Babati wakiwa mafunzoni





Na: Mwandishi wetu,Babati


maipacarusha20@gmail.com


Askari wa wanyamapori katika eneo la Jumuiya ya hifadhi  ya Wanyapori ya  Burunge na askari wa wanyamapori halmashauri ya Babati, mkoa Manyara, wameanza kujengewa uwezo jinsi ya ukamataji wa majangili, kupeleleza na kufanya upekuzi.


Mafunzo ya askari hao, yameandaliwa na Mamlaka ya Usimamizi wanyamapori nchini(TAWA) na kudhaminiwa na Taasisi ya chem chem association, ambayo imekuwa ikiendesha shughuli za Utalii na uhifadhi  katika eneo la Burunge WMA.


Wakitoa mafunzo hayo, Mwendesha mashitaka wa TAWA, Getrude Kariongi na  mwendesha mashitaka kutoka ofisi ya Mkurugenzi wa mashitaka(DPP) mkoa wa Manyara, Brandina Msawa waliwataka askari hao,kuzingatia sheria katika ukamataji wa majangili.


Kariongi alisema kama Askari hao  wakikamata majangili na kufanya upekuzi vizuri na kuhifadhi vizuri ushahidi kesi za ujangili zitasikilizwa kwa wakati na hukumu kutolewa.


 Msawa aliwataka Askari hao, kuzingatia sheria katika ukamataji, upelelezi na upekuzi ili kurahisisha mwenendo wa kesi za ujangili katika maeneo yao.


Awali Afisa Mhifadhi kutoka TAWA Kanda ya kaskazini,  Emmanuel Pius alisema mafunzo hayo ni muhimu kwa askari hao, ili kuimarisha vita dhidi ya Ujangili.


Alisema Maafisa hao, pia watapatiwa elimu na polisi idara ya upelelezi jinsi ya kutoa ushahidi mahakamani na hivyo, kurahisisha usikilizwaji wa kesi.


Pius alisema ni jukumu la askari hao, kuhakikisha wanaendelea kuzilinda maliasili za Taifa kwa faida ya sasa na vizazi vijavyo.


Mkuu wa idara ya Ulinzi ya taasisi ya Chemchem association, Erick Nayman alisema eneo la Burunge WMA kumekuwepo na matukio ya ujangili kutokana na ongezeko shughuli za kibinaadamu ndani ya hifadhi.


Hata hivyo, alisema Chem chem kwa mwaka imekuwa ikitumia zaidi ya shilingi 400 milioni katika kupambana na matukio ya ujangili, ikiwepo ununuzi wa magari na vifaa vya ulinzi .


 Katibu Tawala wilaya ya Babati, Khalfani Matipula akifungua mafunzo hayo, aliwataka askari wa wanyamapori kufanyakazi kwa weledi ili kuhakikisha rasilimali za taifa zinalindwa.


Alisema ni lazima vitendo vya ujangili vikomeshwe katika wilaya hiyo kwa kuhakikisha watuhumiwa wanatakamatwa na kufikishwa mahakamani kwa wakati.




No comments: