BODI ya Ushauri ya Wizara kwa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) wametembelea Hifadhi ya Mazingira Asilia Amani iliyopo Muheza mkoani Tanga lengo likiwa ni kukagua uboreshaji wa miundombinu na huduma za kiutalii ambapo imelidhishwa na hatua iliyofikiwa pamoja na uwekezaji uliofanyika.
Wakati wa ziara hiyo wajumbe wa bodi walilidhishwa na uwekezaji mkubwa uliofanyika wa miundombinu na mazingira ya hifadhi uliofanywa na fedha za Uviko 19 lakini pia bajeti binafsi kuboresha maeneo yaliosalia.
Akizungumza mara baada ya kukagua miradi na vivutio vya utalii vya hifadhi hiyo, mjumbe wa Bodi Wakili Msomi Piensia Christopher Kiure aliupongeza uongozi wa TFS kwa uwekezaji mkubwa waliofanya kwenye hifadhi hiyo na kuutaka kuongeza ubunifu katika kuitangaza hifadhi hiyo.
Amesema uwekezaji mkubwa umeshafanyika na sasa ni wakati wa kuhakikisha kunakuwepo na mikakati thabiti ya kujitangaza huku akiwataka maafisa utalii kuwa wabunifu na kusimamia utekelezaji wa malengo kwa hali yoyote.
“Uwekezaji uliofanyika hapa ni mkubwa sana, hifadhi ina vivutio vingi na miundombinu imeimarika ongezeni nguvu ya kuitangaza, maafisa utalii, wengi wenu ni vijana onyesheni mnatosha, kuweni wabunifu, toeni mawazo na muwe tayari kuyasimamia, na sio lazima lazima uwe na fedha kuanza hili,” anasema Wakili Msomi Kiure.
Aidha, Wakili Msomi Kiure aliutaka uongozi kuingia mikataba (MOU) na nchi zinazofanya vizuri kwenye utalii ikolojia ili kuwe na utaratibu wa kubadirishana wataalamu lengo likiwa ni kubadirishana ujuzi.
Kwa upande wake, Mjumbe wa Bodi CPA. Bahati Lucas Masila aliupongeza uongozi wa TFS kwa kuhifadhi na kuhakikisha miundombinu ya utalii hifadhini hapo inaboreshwa na kuahidi kutumia sehemu ya likizo yake kudhuru na familia yake kupumzika kwa kile alichosema kuvutiwa na hali ya utulivu.
Someni Mteleka ni Mkuu wa Kitengo cha Utalii TFS anasema katika kuhakikisha uwekezaji uliofanyika unakuwa wenye tija, pamoja na mambo mengine tayari wameandaa video za lugha nne tofauti (Kichina, Kijerumani, Kingereza na Kiswahili) lengo likiwa ni kuwafikia watalii wengi zaidi huku wakifungua njia ya Amani kwenda Hifadhi ya Nilo iliyopo Lushoto.
Naye Naibu Kamishana Msaidizi TFS na Mhasibu Mkuu Peter Mwakosya anasema katika mwaka huu wa fedha, Wakala imetenga fedha kwa ajili ya kuboresha zaidi hifadhi zake ili kuwavutia watalii wengi zaidi na hivyo kuchangia katika kufikia idadi ya watalii 5,000,000 hadi ifikapo 2025 iliyowekwa na Serikali huku mapato yakiongezeka. Tulizo Kilaga anaripoti.
No comments:
Post a Comment