BODI YA WAKURUGENZI WA NGORONGORO YATEMBELEA BUSTANI YA WANYAMAPORI YA IFISI, JIJINI MBEYA - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Monday 6 March 2023

BODI YA WAKURUGENZI WA NGORONGORO YATEMBELEA BUSTANI YA WANYAMAPORI YA IFISI, JIJINI MBEYA

  






NA: MWANDISHI WETU

maipacarusha20@gmail.com

BODI ya Wakurugenzi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro ( NCAA)  ikiongozwa na Mwenyekiti wake Jenerali Venance Mabeyo ( Mstaafu)  wametembelea  Bustani ya Wanyamapori  iliyopo katika eneo la Ifisi Jijini Mbeya ambapo katika ziara hiyo wamefurahishwa na Uwekezaji huo.


Bodi hiyo pia  ilipata fursa ya kutembelea  moja ya  Makumbusho ya urithi wa utamaduni ambayo  imesheheni mikusanyo ya aina  mbalimbali ya  makabila ya Nyanda za Juu Kusini ambayo ina  inavifaa vya waganga wa jadi vya kishirikina  ambayo ni sehemu ya utamaduni wa watu wa Nyanda hizo.


Wakati wa ziara hiyo Mwenyekiti Mabeyo  amefurahishwa na jitihada za Mkurugenzi Mshauri wa Kanisa la Uinjilisiti ambaye ni Muanzilishi wa Bustani ya wanyamapori hai, Markus Lehner kwa usimamizi mzuri wa  kulifanya eneo hilo kuwa la kipekee na lenye mvuto wa namna yake kwa watalii


Kufuatia hatua hiyo  ya uwekezaji, Mwenyekiti  huyo  ametoa pongezi kwa Uongozi wa Bustani hiyo kwa  hatua ilizozichukua za kuhifadhi na  kuenzi utamaduni wa watu wa Nyanda za Juu Kusini kwa kufungua Makumbusho hiyo ambayo mbali ya kuwa kivutio cha utalii lakini pia  ni kioo cha kujitazama kama Taifa tumetoka wapi na tunaelekea wapi . 



Amesema ni wakati sasa wa Taasisi na watu binafsi kufungua Makumbusho nyinginezo kwa lengo la kuhifadhi na kuenzi utamaduni wetu kwa faida ya kizazi cha sasa na kijacho.


Kwa upande wake, Mkurugenzi Mshauri wa Kanisa la Uinjilisiti  ambaye ni Muanzilishi wa Bustani ya wanyamapori hai, Markus Lehner amewaeleza Wakurugenzi wa Bodi hiyo kuwa anapenda Uhifadhi wa wanyamapori huku akisisitiza kuwa amekuwa  akitumia muda mwingi kuhakikisha miundombinu ya utalii inaboreshwa ili kuwafanya  watalii wanapotembelea eneo hilo wanafurahia na wanakuwa Mabalozi wazuri kwa watalii wengine.


" Nina wanyama wa kila aina wakiwemo simba, chatu, nyumbu pamoja ndege mbalimbali ili kuhakikisha uwekezaji huu unakuwa endelevu nimesomesha vijana wenyeji wa maeneo haya ambao ndio wamekuwa nguzo ya kuhakikisha kila kitu kinakwenda sawa" amesisitiza


Lengo kuu la ziara hiyo  ni kujifunza ikiwa ni Mkakati wa Bodi hiyo kuhakikisha NCAA inafungua Bustani ya Wanyamapori  katika eneo la Kimondo cha Mbozi ili watalii wakifika katika  eneo hilo wakute vitu vingi vya kutembelea.


Bustani hiyo ya wanyama hai pamoja na Makumbusho hiyo imekuwa ikiwavutia watalii wengu kutembelea kwa vile ni  eneo ambalo Watalii hutumia  muda mwingi wa kuona  vivutio vingi vya utalii kwa wakati mmoja.

No comments: