Mawakili wakizungumza na Waandishi wa Habari |
Mwandishi wetu, Maipac
maipacarusha20@gmail.com
Hatma ya kesi ya kulazimishwa kupotea Mzee Oriais Oleng'iyo mkazi wa Ololosokwani tarafa ya Loliondo itajulikana Mei 10,2023.
Mahakama Kuu ya Tanzania,Masijala ya Arusha, Leo imesikiliza maombi madogo yaliyoletwa na Ndoloi Oriais ambaye kupitia Mawakili wake imewataka wajibu maombi kwa ujumla wao kumleta, kumuachilia au kusema popote alipo Mzee Oriais Pasilange Oleng'iyo(85).
Wajibu maombi ni pamoja na Kamanda wa jeshi la polisi (RPC), Mkuu mkoa wa Arusha, Mkuu wa wilaya na OCD Ngorongoro, Mkuu wa jeshi la polisi(IGP) na Mwanasheria Mkuu wa serikali.
Mbele ya Jaji Mohamed Gwae,Wakili wa mleta maombi, Saimon Mbwabwo aliieleza kuwa Juni 9,2022 huko katika kitongoji cha Nailowa kata ya Ololosokwani na kijiji cha Ololosokwani katika tarafa ya Loliondo wilayani Ngorongoro, askari polisi waliokuwa wakitoa ulinzi kwa maafisa wanaoweka alama za mipaka huku zoezi la kuwaamisha baadhi ya wakazi likiendelea huku wengine wakipinga zoezi hilo kifanyika ndipo yalipotokea machafuko kati ya wananchi na polisi
Aliieleza mahakama hiyo kuwa katika vurugu hizo zilizokuwa zifanyika karibu na makazi ya Oriais baada ya mabishano ya polisi na wananchi wengine huku yakiendelea kusogea nyumbani kwake Mzee huyo alikuwa hausiki na Vurugu hizo lakini alipigwa na risasi na mmoja wa askari ambaye hakujulikana
Alisema kuwa muombaji huyo alikimbia eneo la mlimani kutokana na vurugu iliyokuwepo wakiwa kwenye maficho ya mlimani ndipo alipomuona Mzee Oriais akichukuliwa na Askari polisi na kuondoka nae akiwa amepata jeraha
"Hata hivyo pamoja na Mzee Oriais pia kukamatwa na watu wengine 19 ambao baadhi yao walifikishwa mahakamani kutokana na kukabiliwa na mauaji ya askari polisi hakuletwa mahakamani,"alidai.
Wakili huyo aliiambia mahakama kuwa kabla ya hao waliokamatwa kufikishwa mahakamani walikuwa hawajulikani baada ya siku kadhaa ambao mawakili wao walileta maombi kama haya ambaye Mzee Oriais alikuwa mmoja wao.
"Nawalipoletwa mahakamani ya watu 19 lakini Mzee huyo hakuletwa mahakamani ya hakimu mkazi Arusha lakini watu waliendelea kuongezwa kidogokidogo hadi kufikia 27 tukiamini katika muendelezo huo pengine mzee huyo angeweza kuletwa,"alisema
Wakili huyo aliongeza kuwa baada ya shauri namba 11/2020/2022 kuondolewa 22,11.2022 mahakamani na Jamuhuri ndipo walipogundua kuwa mzee huyo hataletwa tena na ndipo ilipowalazimu kukimbilia mahakamani ili aweze kuletwa kama yupo hai au amefariki.
Alidai kuwa Mzee Oriais wakati anashikiliwa alikuwa eneo la Ololoswokwan lakini kwa namna yeyote endapo atakuwa ameshikiliwa itakuwa kinyume na kifungu namba 391kifungu kidogo cha kwanza(a)(b) cha sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai sura ya 20 kutokana na polisi hawana mamlaka ya kukaa na mtuhumiwa kwa muda wa miezi 9.
Kwa upande wa mjibu maombi (Jamhuri) uliowakilishwa na Wakili Peter Mseti,alipinga maombi hayo kwa kudai kuwa hakuna mahali walalamikaji waliposema namba ya polisi, au namba ya gari ya polisi zaidi ya kusema "difenda" kwani gari hizo zipo nyingi nchini.
Wakili Mseti alidai kuwa hawajawahi kumshikilia mtu huyo, wala jina lake halijawahi kuonekana kwenye majina ya walioshikiliwa kuanzia tarehe 8 hadi 20 ya mwezi tajwa kati ya wale waliokuwa na kesi ya mauaji.
"Mleta maombi ameshindwa kuthibitisha kuwa anayeshikiliwa isivyokihali yupo jela pamoja na kutokupeleka malalamiko kwenye vyombo kama polisi ya kupotea kwa mtu,"alidai Mseti
Akijibu hoja za upande wa jamhuri, Wakili Mbwabwo amesema kwa mazingira ya watu wengi na vurugu zilizokuwepo isingekuwa rahisi kutambua namba ya polisi wala gari.
"Na hoja ya kutokutoa taarifa ya kupotea kwenye vyombo vya dola wasingeripoti kupotea wakati alikamatwa na wanaamini yupo kwenye mikono ya polisi na polisi ndio watuhumiwa ndio maana wameamua kwenda mahakamani wakiamini haki itapatikana,"alisema
Baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili Jaji Gwae amesema atatoa uamuzi mdogo Mei 10,mwaka huu .
No comments:
Post a Comment