NA: JULIETH MKIRERI, MAIPAC KIBAHA
maipacarusha20@gmail.com
WAZIRI wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Innocent Bashungwa amesema Wizara yake itaendelea kuhakikisha inajenga sekta ya Viwanda ili kuendana na muelekeo wa Rais Samia Suluhu Hassan na maelekezo yake katika kutekeleza dira ya uwekezaji.
Waziri Bashungwa ameyasema hayo alipokuwa akikabidhi magari matatu ya zimamoto kwa Wizara ya Mambo ya ndani ambayo yameundwa na Shirika la Tanzania Automotive Technology Centre(TATC) la Nyumbu lililopo Kwamatias Kibaha.
Akizungumza katika hafla fupi iliyohudhuriwa na Naibu Waziri Mambo ya ndani Jumanne Sagini, Makamu mwenyekiti Kamati ya kudumu ya Bunge Mambo ya nje Ulinzi na Usalama, Katibu Mkuu wa Wizara ya Ulinzi na JKT pamoja na viongozi wa Jeshi la zimamoto alisema zipo fursa za uwekezaji katika Wizara ya Ulinzi.
Waziri Bashungwa alisema zipo sekta za uwekezaji katika shirika la TATC la Nyumbu na Mzinga ambayo yako mstari wa mbele kuhakikisha dira hiyo ya serikali inatekelezwa.
"Katika muelekeo huu kwa mashirika haya mawili ambayo yaliasisiwa na baba wa Taifa niwathibitishie kwamba dira ya serikali ya awamu ya sita katika sekta ya ulinzi zipo fursa za uwekezaji na mashirika haya Mzinga na TATC Nyumbu yako mstari wa mbele kuhakikisha dira hii ya uwekezaji tunaitekeleza" amesema.
Bashungwa amepongeza Shirika la Nyumbu kwa namna walivyoshirikiana naJeshi la zimamoto katika kutengeneza magari hayo ambayo yanaenda kusaidia majeshi katika kutimiza wajibu wao.
Akizungumza baada ya makabidhiano ya magari hayo matatu Naibu Waziri Mambo ya Ndani Jumanne Sagini amesema Jeshi la zimamoto linaenda kuwa imara zaidi na kwenda kuzima majanga ya moto pale yanapotokea kutokana na uwepo wa magari hayo.
Amepongeza Jeshi la TATC Nyumbu kwa kutengeneza magari hayo na kwamba tukio hilo ni muendelezo wa ushahidi wa serikali katika kuviwezesha vyombo vya usalama kutekeleza majukumu yake ya msingi na kuviondolea kero ya muda mrefu ikiwemo ya kuboresha mazingira na utendaji wake wa kazi.
Makamu Mwenyekiti Kamati ya kudumu ya Bunge Mambo ya nje Ulinzi na Usalama Vicent Mbogo amesema shirika hilo linatakiwa kujitangaza lakini pia kuainisha vikwazo walivyonavyo ili itafutwe namna ya kuboresha liweze kufanya kazi kwa ufanisi.
Awali akizungumza katika hafla hiyo Mkurugezi Mkuu wa Shirika la Nyumbu Brigedia Jenerali Hashim Komba amesema shirika hilo limekamilisha mkataba walioingia na Jeshi la zima moto wa kuunda magari matatu.
Brigedia Jenerali Komba amesema mara nyingi magari ya zimamoto yamekuwa yakinunuliwa kutoka nje ya nchi na kwamba mradi huo utasaidia pia kupunguza gharama za kufanya natengenezo kutokana na kutengenezwa ndani ya nchi.
No comments:
Post a Comment