Na: Mwandishi wetu
Wanawake wajawazito na watoto wachanga wa mikoa mitano ya Manyara, Tabora, Mwanza, Shinyanga na Geita, watanufaika na mradi wa kitita cha uzazi salama, wenye lengo la kupunguza vifo vyao kwa asilimia 50.
Mradi huo kitita cha uzazi salama ni wa miaka mitatu uliodhaminiwa na benki ya dunia umegharimu dola za kimarekani milioni 4.5 kiasi cha shilingi 11 bilioni na kila mkoa utakuwa na vituo sita.
Mkurugenzi mtendaji wa hospitali ya rufaa ya Haydom wilayani Mbulu, mkoani Manyara, Dk Paschal Mdoe amesema mradi huo utahudumia vituo 30 katika mikoa mitano.
Dk Mdoe amesema kupitia mradi huo wa kitita cha uzazi salama, vifo vya watoto na wanawake wajawazito vya ndani ya saa 24 vitapungua.
Amesema kupitia mradi huo vifo vya watoto wafu vimepungua kwa asilimia 25 kwenye vituo vyote na vifo vya wanawake wajawazito wakati wa kujifungua hasa kwa kutokwa damu nyingi vimepungua kwa zaidi ya asilimia 10.
“Watoa huduma wamehamasika pia kwani wamepata vifaa, wamepata aina bora ya mafunzo na hasa wakunga na wauguzi, ile tabia ya kumuita daktari imepungua kwani wamekuwa na uwezo zaidi,” amesema Dk Mdoe.
Amesema wakunga hao na wauguzi wamekuwa na hali hiyo kutokana na ujuzi walioupata na pia wana vifaa vya kutosha kutokana na mradi wa kitita salama.
Naibu Waziri wa Afya, Dk Godwin Mollel amesema mradi huo wa kitita cha uzazi salama, kitakuwa na manufaa makubwa kwa wanawake na watoto wa mikoa hiyo.
Mkuu wa wilaya ya Mbulu Kheri James amesema kupitia hospitali ya rufaa ya Haydom, watoto na wanawake wajawazito wa Mbulu na Manyara kwa ujumla watanufaika.
Mwanamke mjamzito mkazi wa Haydom, Rose Umbay ameishukuru serikali kwa kufanikisha mradi huo kwani kwa namna moja au nyingine utakuwa na manufaa kwao.
No comments:
Post a Comment