Na: Mwandishi wetu
maipacarusha@gmail.com
Meatu.Wizara ya Ardhi imeanza kupima Vijiji 12 ambavyo vinaunda Jumuiya ya hifadhi ya wanyamapori ya Makao(Makao WMA), ili kuwa na mpango wa matumizi bora ya ardhi na hivyo kupunguza uvamizi wa maeneo yaliyohifadhiwa.
Mpango huo pia unatarajiwa kusaidia kupunguza migogoro baina ya wanyamapori hasa Tembo na wananchi katika wilaya ya Meatu,kutokana na mara kadhaa Tembo kuvamia mashamba na makazi ya watu.
Afisa Wanyamapori wilayani Meatu, Deusdedit Martin akizungumza na mwandishi habari hizi, alisema kupimwa kutakuwa na manufaa makubwa kwa vijiji.
"sasa vijiji vyetu, vitajipanga vizuri kwa kutenga maeneo ya kilimo,makazi, michezo na shughuli za uhifadhi"alisema.
Alisema wilaya hiyo,ina mikakati ya kuboresha shughuli za uhifadhi na Utalii,lakini pia kuhakikisha migogoro baina ya wanyamapori na wananchi inapungua.
Akizungumzia changamoto ya ongezeko la Tembo kwenye makazi wa watu katika wilaya hiyo, alisema tayari halmashauri hiyo kwa kushirikiana na wadau wa uhifadhi inaendelea kutoa elimu juu kuzuia Tembo kufika katika maeneo ya makazi ya watu.
mkazi wa kijiji cha Makao Julius Yohana alipongeza serikali, Makao WMA na mwekezaji kampuni ya Mwiba, kuwezesha mpango wa kupimwa vijiji vyao na kuwa na mpango wa matumizi bora ya ardhi.
Yohana amesema, vijiji vyao vimekuwa vikinufaika sana na uhifadhi, ikiwepo kupata fedha za miradi mbali mbali, ikiwepo kujengewa shule, vituo vya afya, kupata mikopo midogomidogo na kufanya shughuli za ujasiriamali.
Katika Jumuiya ya hifadhi ya wanyamapori ya MAKAO, kuna mwekezaji taasisi ya Mwiba Holding ltd ambayo imekuwa ikifanya shughuli za utalii wa picha ikiwepo hoteli ya kitalii ya kifahari ambayo imekuwa ikitembelewa na wageni maarufu duniani.
No comments:
Post a Comment