CMSA YAWAJENGEA UWEZO WAJASIRIAMALI KANDA YA KASKAZINI - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Thursday 22 June 2023

CMSA YAWAJENGEA UWEZO WAJASIRIAMALI KANDA YA KASKAZINI

 



Na Mwandishi wetu, Arusha

maipacarusha20@gmail.com


MAMLAKA ya masoko na mitaji ya dhamana (CMSA) imewajengea uwezo wajasiriamali wa kanda ya kaskazini ili kutambua masoko ya mitaji kwa maendeleo ya uchumi.


Mkurugenzi wa mawasiliano, mamlaka ya masoko ya mitaji na dhamana (CMSA) Charles Shirima akizungumza kwenye semina ya kuwezesha wajasiriamali jijini Arusha amesema elimu hiyo ni mpya kwa wajasiriamali wengi.


Shirima amesema CMSA imeanza mpango mkakati wa kutoa elimu ya kuwawezesha wajasiriamali wadogo na wa kati namna ya kuandaa miongozo ya upatikanaji wa mitaji halaiki kwa lengo la kuwekeza ili kujiinua kiuchumi.


"Lengo letu ni kuhakikisha wajasiriamali wa kati na wadogo wanapata elimu ya upatikanaji wa mitaji kuhusu uandaaji wa miongozo ya ushiriki katika mitaji halaiki," amesema Shirima.



Amesema mfumo huo utasaidia kusimamia biashara ndogo na kati na utasaidia kukusanya fedha za mitaji ya biashara ndogo na kati kwa ajili ya shughuli za uwekezaji kwa kupitia mfumo wa mtandao ambazo zitakuwa zinasimamiwa CMSA ambayo imepewa usimamizi kisheria.


Amesema huo ni mfumo mpya ambao hapo awali haukuwepo nchini Tanzania na wameanza kutoa leseni katika kipindiki hiki ikiwa katika masoko mengine ya nchi jirani wao walianza muda mrefu.


Amesema hiyo ni moja ya utekelezaji wa sera za serikali katika kuziwezesha wafanyabiashara wadogo na wakati, njia ya kupata mitaji na kuchangia katika ukuaji wa uchumi.


"Kwa hiyo tuna matumaini kwamba kwa kutoa elimu hii itawasaidia wawekezaji wadogo na wakati katika kukuza biashara zao na kukuza kipato cha Taifa na mtu mmoja mmoja," amesema Shirima.


Mmoja wa wakufunzi  wa taasisi ya elimu ya biashara kwa vijana na uwekezaji (ICESA- Africa) Geofrey Julius amesema fursa hiyo mpya itaongeza chachu katika uzalishaji wa bidhaa mbalimbali hali ambayo itaruhusu vijana kujiajiri na kuwa suluhisho la upatikanaji wa mitaji.


Mshiriki wa mafunzo hayo Baraka Gaspa ametoa wito kwa vijana kuwa ni vyema wakafuatilia mamlaka hiyo ili kupata taarifa sahihi za uwekezaji kwa lengo la kujiendeleza kiuchumi.


Mshiriki mwingine wa mafunzo hayo Regina Mlay wa jijini Arusha, amesema mafunzo hayo yatawasaidia katika kuwajenga na kujiimarisha kiuchumi kwani awali hawakuwa na elimu hiyo ya uwekezaji.



No comments: