MAHAKAMA YA AFRIKA YA HAKI ZA BINADAMU NA WATU KUTOA MAAMUZI KUHUSU SHERIA INAYOZUIA DHAMANA NCHINI TANZANIA - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Tuesday 13 June 2023

MAHAKAMA YA AFRIKA YA HAKI ZA BINADAMU NA WATU KUTOA MAAMUZI KUHUSU SHERIA INAYOZUIA DHAMANA NCHINI TANZANIA

 


Na Mwandishi wetu ARUSHA


maipacarusha20@gmail.com


Leo 13 Juni 2023 kuanzia saa 4:00 za asubuhi, Mahakama ya Afrika Juu ya Haki za Binadamu na Watu itatoa maamuzi kuhusu shauri la maombi namba 039/2020 linalopinga kifungu cha 148(5) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai kinachozuia Mahakama kutoa dhamana kwa watuhumiwa wa baadhi ya makosa ya jinai

Ikumbukwe 18 Novemba 2020 Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kwa pamoja walifungua shauri la maombi namba 039/2020 katika Mahakama ya Afrika Juu ya Haki za Binadamu na Watu kupinga kifungu cha 148(5) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai.

 Kifungu hicho kina orodha ya makosa ambayo hayana dhamana kama vile; mauaji, uhaini, ugaidi, utakatishaji fedha, n.k. 

Kesi hii ilifunguliwa baada ya Mahakama ya Rufani nchini Tanzania kutoa maamuzi kwamba kifungu hicho hakikiuki Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwenye rufaa namba 175 ya mwaka 2020 [Mwanasheria Mkuu wa Serikali dhidi ya Dickson Sanga]


Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilitunga sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai tarehe 01 Novemba 1985 ikiwa na kifungu cha 148(5) ambacho kimefanyiwa marekebisho mara kadhaa huku makosa yasiyokuwa na dhamana yakizidi kuongezwa katika kifungu hicho. 

Kwa mujibu wa THRDC na LHRC, kifungu cha 148(5) kinapoka mamlaka ya Mahakama katika kusikiliza maombi ya dhamana ya watuhumiwa, kinakiuka haki ya kuwa huru na kuishi kama mtu huru, haki ya kusikilizwa, na haki ya kudhaniwa kuwa mtuhumiwa hana hatia mpaka pale ambapo itathibitika vinginevyo, kama ambavyo haki hizo zinalindwa na Mkataba wa Afrika Juu ya Haki za Biandamu na Watu, Tamko la Ulimwengu juu ya Haki za Binadamu, Mkataba wa Kimataifa juu ya Haki za Kiraia na Kisiasa pamoja na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977.


Kesi nyingine itakayotolewa uamuzi ni kesi ya Bob Chacha Wangwe dhidi ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo inapinga Vifungu vya Sheria ya Taifa ya Uchaguzi ambvyo vinaruhusu wakurugenzi kuwa wasimamizi wa uchaguzi wakati ni makada wa Chama Cha Mapinduzi ambacho ni chama tawala hivyo ni vigumu uchaguzi kuwa wa huru na wa haki, lakini pia vifungu hivyo vinakiuka haki ya usawa mbele ya sheria ikiwa ni pamoja na haki ya wananchi kuchagua viongozi wao wanaowataka kwa uhuru.


Imetolewa na

Tanzania Human Rights Defenders Coalition (THRDC)

June 12, 2023

Arusha, Tanzania

No comments: