NA: ANADREA
NGOBOLE, ARUSHA
MAHAKAMA ya Afrika
ya haki za binadamu leo imetolea maamuzi mashauri tisa yaliyofunguliwa katika
mahakama hiyo ambapo katika mashauri hayo tisa mashauri nane yalikuwa dhidi ya
serikali ya Tanzania.
Miongoni mwa
mashauri yaliyotolewa maamuzi na mahakama hiyo ni shauri namba 11/2020 lililofunguliwa
na kituo cha sheria na haki za binadamu kwa kushirikiana na Bob Chacha Wangwe
kupinga sheria ya uchaguzi inayowaidhinisha wakurugenzi wa halmashauri kuwa
wasimamizi wa uchaguzi.
Katika shauri hilo
wafungua shauri waliwakilishwa na mawakili Furgence Masawe, Jebra Kambole,
Paulo Kisabo na Amani Joachim na kwa upande wa serikali iliwakilishwa na wakili
Mkama Musalamu na Christabella Madembwe kutoka ofisi ya mwanasheria mkuu wa
Serikali.
Hoja ya msingi kupinga kifungu hicho kwa
wafungua shauri ilikua ni kwamba wakurugenzi wa Halmashauri wanavinasaba vya
kisiasa kwa kuwa wao ni wateule wa Rais
lakini pia haijaanishwa sifa tofauti katika uteuzi wao zinazowawezesha kuwa na
sifa za kuwa wasimamizi wa uchaguzi ambao
utakua huru na haki.
Akisoma hukumu
hiyo mahakamani hapo Jaji Dennis Dominic Adjei amesema kwa pamoja majaji hao
wamekubaliana na hoja za wapeleka maombi kwa hoja walizoziwasilisha na maamuzi
ya mahakama hiyo ikatoa miezi 12 kwa serikali ya Tanzania kubadili kifungu
hicho kinachotumika kuteua wakurugenzi kuwa wasimamizi wa uchaguzi na kuiagiza
serikali ya Tanzania ndani ya miezi sita kuwasilisha taarifa katika mahakama hiyo
imefikia hatua gani katika kutekeleza maamuzi hayo ya mahakama.
Maamuzi hayo ya
mahakama ya Afrika ya haki za binadamu yameendana na hukumu ya awali
iliyotolewa na mahakama kuu kuhusiana na
shauri hilo lilipofunguliwa katika mahakama kuu na baadae serikali kukata rufaa
mahakama ya Rufaa ya Tanzania na mahakama hiyo kutengua uamuzi wa mahakama kuu
hali iliyopelekea Wangwe na LHRC kuamua kupeleka shauri hilo mahakama ya Afrika
ambayo leo imelitolea maamuzi.
Mahakama hiyo pia ilitolea uamuzi shauri namba 039/2020 lililofunguliwa na kituoa cha sheria na haki za
binadamu kwa kushirikiana na Mtandao wa watetezi wa haki za binadamu Tanzania
ambapo walifungua shauri dhidi ya serikali ya Tanzania kupinga kifungu cha sheria
ya makossa ya jinai namba 145 kifungu kidogo cha 5 kinachonyima haki ya
mtuhumiwa kupata dhamana.
Kifungu hicho
kimeanisha makossa mbalimbali ambapo katika makossa hayo kuna makossa yametajwa kutokua na dhamana pindi mtu
anapotuhumiwa kuyatenda.
Katika shauri hilo
wapeleka maombi walitoa sababu za kupinga kifungu hicho kuwa kinakiuka haki za
binadamu na pia kinaingilia uhuru wa mahakama katika kuendesha mashauri
mahakamani kwa mtuhumiwa kuwekwa ndani hata kabla ya mahakama kumthibitisha kuwa
ana hatia.
Mahakama katika
kupitia shauri hilo majaji wa mahakama hiyo wamejiridhisha kuwa kifungu hicho
kinakiuka misingi ya haki za binadamu na hivyo kuiagiza serikali ya Tanzania
kukifanyia marekebisho kifungu hicho na kuhakikisha marekebisho hayo yanawekwa
katika tovuti ya Mahakama, mbao za matangazo za mahakama ili wananchi
wote kuelewa mabadiliko hayo.
Akizungumza mara
baada ya maamuzi hayo ya mahakama kutolewa wakili Jebra Kambole alisema hiyo ni
hatua kubwa kufikiwa kwa nchi hivi sasa wakati Rais akiwa ameunda tume ya haki
jinai kwa dhamira ya kuhakikisha kunafanyika maboresho makubwa ya sheria za
haki jinai.
Kambole alifafanua
kuwa tume hiyo inapaswa sasa kutumia uamuzi huo wa mahakama kuishauri serikali
kutekeleza kwa haraka ili dhamira njema ya Rais kwa nchi yake kuwezesha
wananchi kupata haki wanazostahili itimie.
No comments:
Post a Comment