NA: MWANDISHI WETU ARUSHA
maipacarusha20@gmail.com
Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Innocent Bashungwa amewataka wahitimu wa Mafunzo ya Kozi ya Ukamanda na Unadhimu kwenda kutumia ujuzi walioupata kusaidia ulinzi na amani katika nchi zao.
Maafisa wa jeshi 65 kutoka nchi 12 barani Afrika wakiwepo watanzania 49 walihimu mafunzo hayo katika mahafari yaliyofanyika juzi, katika chuo cha Ukamanda na Unadhimu, Duluti wilayani Arumeru, mkoani Arusha.
Maafisa hao, licha ya kuhimu mafunzo hayo ya kijeshi pia,walihitimu shahada ya uzamili katika masuala ya ulinzi na usalama na baadhi astashahada katika masuala ya ulinzi na usalama.
Akizungumza katika mahafari hayo ya kundi la 37/22-23, Waziri Bashungwa alisema kazi ya jeshi ni kazi ambayo imetukuka kutokana na kuwa na jukumu kubwa la ulinzi na usalama katika nchi.
Alisema anaimani wahitimu wa mafunzo, hayo watakwenda kuboresha utendaji wa kazi katika nchi zao na kuimarisha utendaji wa kazi na weledi katika masuala ya ulinzi na usalama.
“Mafunzo haya pia yanaimarisha mahusiano baina ya nchi mbali mbali katika masuala ya demokrasia ya ulinzi na urafiki uliopo”alisema
Waziri Bashungwa aliwatunuku Wahitimu 65 Hadhi ya psc (Pass Staff College) na kuwakabidhi vyeti na zawadi kwa washindi waliofanya vizuri.
Awali, Mkuu wa Chuo cha Ukamanda na Unadhimu, Brigedia Jenerali Sylvester Damian Ghuliku, aliwapongeza Wahitimu na kuwatakia kila la heri wanaporejea kwenye vituo vyao vya kazi.
“Tunawahakikishia kuwa Chuo kinaona fahari na kujivunia maarifa mliyopata mtakwenda kuyatumia vizuri katika nchi zenu na katika vituo vyenu vya kazi”alisema
Akitoa maelezo ya Kozi ya Ukamanda na Unadhimu, Kundi la 37/22-23, Mkufunzi Mkuu, Kanali Khaji Maulid Mtengela, alisema Wahitimu wote wamefuzu na kufikia viwango vilivyowekwa, hivyo wanastahili kutunukiwa hadhi ya psc.
Wahitimu wa mafunzo hayo, walitoka nchi za Burundi, Malawi,Uganda, Uswatini,Afrika kusini, Misri, Nigeria,Msumbiji, Rwanda,Kenya, Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Wenyeji Tanzania.
No comments:
Post a Comment