MCHENGERWA ATANGAZA MAZAO 3 YA UTALII YANAYOPATIKANA TANZANIA PEKEE, DUNIANI - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Tuesday 13 June 2023

MCHENGERWA ATANGAZA MAZAO 3 YA UTALII YANAYOPATIKANA TANZANIA PEKEE, DUNIANI

 




Na Mwandishi wetu 

maipacarusha20@gmail.com

Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mohamed Mchengerwa ametangaza mazao rasmi matatu ya utalii ambayo hayapatikani nchi yoyote duniani isipokuwa Tanzania na kuwaomba watanzania kuyatumia na kuyatangaza ili wageni kutoka sehemu mbalimbali kuja kuona.


Mhe. Mchengerwa ametoa kauli hiyo leo wakati alipokuwa na Katibu Mkuu, Dkt Hassan Abbasi pamoja na Menejimenti ya Bodi ya Utalii nchini kumtangaza  Mwanamitandao ya kijamii maarufu nchini na duniani Nicholas Reynolds maarufu kama Bongozozo ambaye ana mtandao mpana unaojumuisha mabloger mbalimbali wa kimataifa wanaofikia watu zaidi ya milioni 100 duniani.


Waziri  Mchengerwa ameyataja mazao  hayo matatu ya utalii ambayo hayapatikati sehemu yoyote duniani isipokuwa Tanzania  kuwa ni pamoja na tukio la msafara wa Wanyama Numbu katika Hifadhi ya Serengeti  maarufu kama Great Migration, tukio la  kutembea  kwa miguu  kwa wageni  katikati ya Hifadhi ya Ruaha  umbali wa takribani kilomita hamsini na kuwepo kwa  msafara  wa makundi makubwa na kuweka  makazi kwa samaki mkubwa kuliko wote duniani Potwe maarufu kwa jina la Papa Usingizi katika Hifadhi ya Bahari ya Kisiwa cha Mafia.


Amefafanua  kuwa mazao yote  haya matatu  hayapatikani mahali popote duniani isipokuwa  Tanzania ambapo amesema  pamoja na kuwepo lakini  bado watu wengi hawayatambui kwa kuwa hayajatangazwa kikamilifu  hiyo kutoa wito kwa Bodi ya Utalii nchini kutoka na kutangaza  mazao haya  kikamilifu.


“Ndugu zangu ni  vizuri kutambua kuwa Tanzania  ni miongoni mwa nchi chache duniani na ya kwanza Afrika kwa kuwa na  vivutio vingi vya utalii lakini  havijatangazwa  hivyo nitoe wito kwa watanzania  wote kuwa wazalendo na mabalozi wa  kutangaza  na kuthamini urithi huu tuliopewa na Mwenyezi Mungu” amesisitiza Mhe. Mchengerwa


Aidha, amemwomba Bongozozo kuwa balozi mzalendo na bora  wa Tanzania  ili kutumia umaarufu na mtandao wake kuutangaza utalii wa Tanzania kila kona ya dunia ambapo ameitaka Bodi ya Utalii nchini  kupitia orodha ya mabalozi wa heshima  kuona wale wasiofanya kazi na kuwaondoa ili kubaki na wachapakazi.


Kwa upande wake Bongozozo, raia wa Uingereza ambaye ameoa na kuishi Tanzania kwa muda mrefu ameahidi mbele ya Waziri wa Utalii Mhe. Mohamed Mchengerwa na Katibu Mkuu, Dkt. Hassan Abbasi, kuwa atatumia ipasavyo ushawishi wake duniani kuutangaza utalii wa Tanzania. 




Mkurugenzi wa Masoko wa Bodi ya Utalii nchini, Dkt. Glladstone Mlay amesema  kwa  sasa Bongozozo anaanza  ziara yake kutangaza  vivutio  vya utalii  kusini mwa Tanzania ikiwa ni utekelezaji wa Mkakati wa utangazaji utalii kusini mwa Tanzania (Tanzania’s Southern Circuit Marketing and Promotion Strategy 2021-2026) ambao uliandaliwa kupitia mradi wa  REGROW na kuzinduliwa Septemba 2022 Mkoani Njombe umetaja njia mbalimbali za utangazaji utalii wa Kusini mwa Tanzania ikiwa ni pamoja na kutumia; watu maarufu/mabalozi wa hiyari, utangazaji kwa njia ya mtandao (Digital and Social Media Marketing) vyombo vya habari, safari za mafunzo na kushiriki katika maonesho ya kibiashara (Travel Trade Marketing) ,matukio.


“Leo tumekutana hapa ili kuwajulisheni kuwa kuna ziara ya kimafunzo (Fam Trip ) ya BW. NICHOLAS REYNOLDS   maarufu kama Bongozozo, raia wa Uingereza (Enland) kuanzia tarehe 13 Juni ,2023 hadi tarehe 24 Juni ,2023 katika mikoa ya nyanda za juu kusini, Tanzania.” amefafanua 


Ameongeza kuwa Bw. Nick Reymonds (Bongozozo), ni Balozi wa hiari wa utalii (Good will Tourism Ambassador)  tangu mwaka 2019 ambapo amekuwa mstari wa mbele katika kuitangaza Tanzania na vivutio vyake ikiwa ni  pamoja na kutumia michezo ndani na nje ya nchi, kutumia bloggers wenzake maarufu kama (Drew Binsky)   na mbinu nyingine mbalimbali katika kuitangaza Tanzania kikanda na Kimataifa.  


Amesema ziara hiyo itampa fursa yeye kama balozi kufahamu vizuri vivutio kwa uhalisia wake ili kumrahisishia katika utangazaji wake katika maeneo mbalimbali ambayo atatembelea katika utangazaji wake. 


Aidha amesema katika kipindi hiki  cha takribani wiki mbili za   FAM TRIP ya Bongozozo,  mawakala wa utalii wameandaa vifurushi (Package) za kutembelea vivutio hivyo  atakavyotembelea Balozi huyu katika Hifadhi ya Taifa ya Udzungwa, Pori la Akiba la Mpanga Kipengere Hifadhi ya Taifa ya Ruaha na Hifadhi ya Taifa ya Nyerere. 


Waziri Mchengerwa  amewanakaribishwa watanzania wote kujumuika na Bongozozo  katika kutembelea vivutio  vya utalii vya nyanda za juu kusini ambavyo kwa sasa Serikali imeongeza nguvu kupitia mradi wa Usimamizi Rasilimali za Maliasili kwa Utalii na endelevu (REGROW)  na kuendelea kuunga mkono jitihada za Rais wa jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan katika jitihada zake za kutangaza Tanzania kupitia Filamu pendwa ya “Tanzania The Royal Tour”.


No comments: