WAANDISHI WANACHAMA WA MAIPAC SABA WATEULIWA KUWANIA TUZO ZA UMAHIRI WA UANDISHI WA HABARI TANZANIA (EJAT) - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Friday 23 June 2023

WAANDISHI WANACHAMA WA MAIPAC SABA WATEULIWA KUWANIA TUZO ZA UMAHIRI WA UANDISHI WA HABARI TANZANIA (EJAT)



Kajubi Mukajanga Katibu mtendaji wa Baraza la Habari Tanzania akitaja majina ya waandishi walioingia katika tuzo za EJAT 


Andrea Ngobole,Arusha

maipacarusha20@gmail.com


Waandishi wa habari saba wanachama wa Shirika la Wanahabari la  kusaidia Jamii za pembezoni (MAIPAC)  ni miongoni mwa waandishi 91 Kati ya 728 walioteuliwa katika tuzo za EJAT mwaka 2022.


MAIPAC ni taasisi ya wanahabari ambayo imekuwa ikiwezesha wanahabari kufanya habari za uchunguzi, mazingira, utawala Bora na utetezi wa Jamii za pembezoni katika masuala ya Maendeleo.


Waandishi wanachama wa MAIPAC walioteuliwa ni Mkurugenzi wa MAIPAC ,Mussa Juma ambaye ni mwandishi mwandamizi wa gazeti la mwananchi mkoa Arusha.


Wengine ni Anthony Mayunga Afisa Utafiti wa MAIPAC mwandishi mwandamizi wa gazeti la Jamuhuri  mkoa Mara na Elizabeth Edward anayeandikia gazeti la mwananchi jijini Dar es Salaam.


Wengine ni  Janeth Joseph anayeandikia gazeti la mwananchi mkoa Kilimanjaro,Ramadhabi Mvungi wa Azam TV na Profit Manga wa Arusha Leo na Wasafi media na Vumilia Macha WA Savvy FM.




Wateule  hao 91 wametangazwa Leo Jijini Arusha na baraza la Habari Tanzania (MCT) kutokana na kazi 893 ambazo zimetumwa kuingia katika mashindano hayo.


Katibu Mtendaji wa Baraza la Habari Tanzania (MCT) Kajubi Mukajanga amesema kazi zilizopokelewa mwaka huu na MCT  ni ongezeko la kazi 291 kutoka kazi 598 za mwaka 2021.


Kajubi amesema  Kati ya wateule hao 91 , wateule 36 wanaandikia magazeti,27 katika mitandao ya kijamii ,15 wanatoka radio na 13 wanatoka kwenye Luninga.


Amesema washindi wa Tuzo hizo watatangazwa Rasmi Julai 22 katika hafla ambayo itafanyika ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es salaam ambapo mgeni Rasmi anatarajiwa kuwa Jaji Mkuu Mstaafu Jaji Mohamed Chande Othman.


MAIPAC ni shirika la wanahabari ambalo limekuwa na miradi kadhaa ikiwepo mradi wa uhifadhi wa mazingira kwa maarifa ya asili ambazo umefadhiliwa na mfuko wa mazingira Duniani(GEF) kupitia  program ya miradi midogo ya Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP)


MAIPAC pia limekuwa na mradi wa kupinga ukeketaji wilaya ya Longido ambao unadhaminiwa na marafiki wa Shirika hilo wa nchini Canada.


MAIPAC kwa udhamini wa Shirika la Internews pia wamewahi kuwa na mradi wa matumizi sahihi ya mitandao(Digital  Literacy)kwa wanafunzi wa kike wa Elimu ya juu mkoa Arusha .


Katika kuimarisha Utendaji wa wanahabari hasa katika kuandika habari za Haki za binaadamu MAIPAC imekuwa ikiwajengea uwezo wanahabari kwa ushirikiano wa Mtandao wa watetezi wa Haki za binaadamu (THRDC) Shirika la DefendDefenders, Mtandao wa mashirika ya Jamii za wafugaji na waokota matunda(PINGOs forum) na Jumuiko la Maliasili Tanzania (TNRF) na Shirika la Journalist for Human Rights lenye Makao makuu Canada.




No comments: