![]() |
| Mkurugenzi mtendaji wa Mimutie women Organization Rose Njilo akielezea dhamira ya mtandao WA kupinga ukatili wa jinsia kwa jamii za pembezoni |
NA: Andrea Ngobole, Arusha
maipacarusha20@gmail.com
Mashirika yasiyo ya kiserikali mkoa wa Arusha, yameunda
mtandao wa kukabiliana na matukio ya ukatili dhidi ya wanawake na watoto kwa
jamii za pembezoni.
Mtandao huo, unatarajiwa kujihusisha na kutoa elimu
kupinga ukatili dhidi ya wanawake na watoto, kufanya utafiti wa kukomesha ukatili,
kuwaokoa watoto waliofanyiwa ukatili na kuuganisha mashirika hayo na wadau
wengine wa ndani na nje ya nchi katika kukabiliana na ukatili kwa wanawake na
watoto.
![]() |
| Afisa Maendeleo Mkoa wa ARUSHA Blandina Nkini akizungumza Katika uzinduzi WA mtandao huo |
Akizungumza katika uzinduzi wa mtandao huo, Afisa
maendeleo mkoa wa Arusha Blandina Nkini alipongeza Mashirika yasiyo ya
kiserikali mkoa Arusha yakiongozwa na Mimutie women Organization kuungana
kupambana na ukatili wa jinsia ambao unaongezeka kwa kasi nchini.
Ameutaka mtandao huo kuongeza Katika majukumu yao kuwa na mpango wa elimu ya kumlinda mtoto wa kiume asitendewe vitendo vibaya ili
kujenga Taifa imara kwani kuwasahau watoto wa kiume kunapelekea kuwa na kizazi
kisichojitegemea.
Mkurugenzi mtendaji wa shirika la Mimutie Women Organization
Rose Njillo amesema kuwa mtandao huo unaoundwa na mashirika 10 ya utetezi wa
haki za jamii za pembezoni utakuwa chachu ya kufikia malengo ya kupinga ukatili
wa kijinsia hususani ndoa za utotoni na za lazima, ukeketaji kwa watoto wa kike,
vipigo ndani ya ndoa na elimu ya afya ya uzazi kwa wanawake na wasichana wa
jamii za pembezoni.
“Sisi Mimutie Women Organization tumejitahidi sana kupaza
sauti za kupinga ukatili wa jinsia kwa jamii za pembezoni kwa miaka kumi sasa
na ndiyo maana tumeona ni vema sasa kuunda mtandao wa kupinga ukatili huu kwa
jamii hizi ili kuwa na sauti pana Zaidi kwa kushirikiana na mashirika mengine
10 yenye mlengo wa kutetea haki za jamii za pembezoni, naamini kwa pamoja
tutafikia malengo ya kutokomeza ukatili huu kabisa.” Alisema mkurugenzi huyo
![]() |
| Mwenyekiti wa UWT Arusha Flora Zelothe akizungumza na Waandishi wa Habari mara baada ya kuzinduliwa KWA mtandao huo |
Mwenyekiti wa umoja wa wanawake Tanzania (UWT) Mkoa wa
Arusha Flora Zelothe amewapongeza Mimutie Women Organization na mashirika
mengine kumi kuanzisha mtandao huo wa kupinga ukatili wa kijinsia kwa jamii za
pembezoni na kuwataka kushirikiana na Mtakua iliyoanzishwa na serikali ya awamu
ya sita katika kupata taarifa kamili za matendo ya ukatili kwa jamii kuanzia
ngazi ya kitongoji na vijiji ili kupunguza ukatili wa jinsia kufikia asilimia
sifuri Mkoani Arusha.
“Nawapongeza sana mashirikia yasiyo ya serikali mkoani
Arusha mnafanya kazi nzuri na kwa kuwa mmeanzisha mtandao huu basi mtakuwa na
sauti pana zaidi ya kusemea madhara ya ukatili wa jinsia, ukatili kwa watoto na
wanawake ili uweze kwisha kabisa mkoani Arusha”. Alisema
Mkurugenzi wa ANGONET Petro Aham amesema wanafurahi kushirikishwa
na mtandao huu unaoanza kufanya kazi katika mkoa wa Arusha na kuahidi kusaidia kuweka
mpango mkakati wa kufichua na kupinga ukatili wa kijinsia ili kuhakikisha kunakuwa na jamii za pembezoni
inayotambua na kuheshimu haki za binadamu.
Mkurugenzi wa shirika la wanahabari la kusaidia jamii za
pembezoni la MAIPAC, ambao ni miongoni mwa waanzilishi wa mtandao huo, Mussa
Juma alisema lengo kubwa la mtandao ni kusaidia jamii za pembezoni kukabiliana
na ukatili.
“Maipac
tumekuwa na miradi kadhaa kusaidia jamii hii ikiwepo wa mazingira unaodhaminiwa
na mfuko wa mazingira duniani (GEF) kupitia miradi midogo ya shirika la maendeleo
la umoja wa mataifa (UNDP) na karibuni tumekuwa na mradi wa kupambana na
ukeketaji wilaya ya Longido ambao unadhaminiwa na marafiki wetu wa nchini
Canada sasa kupitia mtandao tutafanya kazi kubwa kwa kushirikiana na mashirika
mengine” alisema
![]() |
| Jopha Malulu mkazi WA Mundarara Wilayani Longido |
Naye Jopha Malulu mama wa watoto watatu, Mhanga wa ndoa
za utotoni anasema kuanzishwa kwa mtandao huu utasaidia sana kupunguza ukatili
kwa mtoto wa kike kuozeshwa akiwa bado mdogo, vipigo ndani ya ndoa na kunyimwa
haki ya kupata elimu ili aweze kufikia malengo makubwa kwa watoto wa kike na
kupunguza umaskini kwa jamii hizo.
“Niliolewa nikiwa
na miaka 14 bila ridhaa yangu ila kwa mapendekezo ya wazazi wangu nikiwa
sielewi masuala ya ndoa jinsinya kumhudumia Mume na baadae baada ya kujitambua
na kupigania haki zangu niliachana na Mume wangu na kunyimwa hata sehemu ya
kuishi n ahata kuwaona watoto wangu wawili niliopata na Mume wangu.” Alisema





No comments:
Post a Comment