| Baadhi ya wanafunzi wa sule ya Msingi Orbomba wakibadilishana mawazo nje ya madarasa yao wakati wa mapumziko ya mchana |
| Baadhi ya wanafunzi wa shule ya Msingi Orbomba wakiwa mapumziko |
NA: Andrea Ngobole,
Longido
Kati ya watoto kumi wa
shule ya Msingi Orbomba wilayani Longido Mkoani Arusha ni watoto sita tu ambao
hufika shule na kuhudhuria masomo. Hii ni asilimia arobaini ya watoto wote
wanaotakiwa kufika shule. Njaa imesababisha wanafunzi washindwe kuhudhuria
masomo.
Hali iliyopo katika
shule hii ndiyo picha halisi iliyopo katika
shule za msingi 43 zilizopo wilayani Longido. Vijiji vingi vya wilaya ya
Longido vinakabiliwa na ukame ambao umeleta njaa kali katika
familia kiasi kwamba watoto wanashindwa kwenda shule.
Mwalimu Lekishon
Thomas wa Shule ya Msingi Orbomba anakiri utoro wa
wanafunzi shuleni hapo unaosababishwa na njaa kali. Hata wale wachache wanaohudhuria
masomo, utendaji wao darasani siyo mzuri kwasababu ya njaa. Kuna baadhi
wanahudhuria masomo asubuhi tu, ikifika mchana hushindwa kuvumilia njaa na
kutoroka.
“Kimsingi
mahudhurio ya watoto shuleni hapa ni madogo kutokana na njaa, walimu pia tunashindwa
kuendelea na vipindi vya mchana kwani usikivu na uelewa wa watoto unakuwa mdogo
sana kwa sababu ya njaa,” anasema
Anasema kamati ya shule imepanga kutafuta
chakula kwa wahisani ili waanze kuwapikia wanafunzi hao na baaadae wazazi waje wachange
shilingi 18,000 kwa muhula ili waendelee na utaratibu wa kuwapikia
chakula.
Shule hiyo ina jumla ya wanafunzi 445 ambapo
mahudhurio ni wastani wa asilimia 60 na asilimia 40 hawahudhurii shule kabisa
kutokana na njaa.
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Ngoswaki
Bi. Kwamboka Nyanami naye anakiri kuwa tatizo la njaa linasababisha utoro kwa wanafunzi
wa shule hiyo pia inayopatikana katika Kata ya Engarenaibor wilayani hapo.
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msing Kimokowa, Robert Minja anaainisha changamoto kubwa ya
utoro wa wanafunzi shuleni hapo inasabishwa na njaa. Anaeleza kuwa wazazi pia wana
mwamko mdogo katika kuchangia chakula kwa wanafunzi.
Mwalimu mkuu wa shule ya msingi Ketumbeine
Felix Mungaya amesema njaa ilisababisha sana utoro wa wanafunzi shuleni hapo na
baada ya kugundua hilo waliomba mashirika yasiyo ya serikali kutoa msaada wa chakula
shuleni hapo na kuanza kupika chakula cha mchana na kupelekea utoro kupungua
kwa kiasi kikubwa na kuongeza tija katika ufundishaji na kuongeza ufaulu wa
wanafunzi.
Aidha uchunguzi
uliofanywa na chombo hiki wilayani hapo umebaini kuwa baadhi ya watoto
wanaosoma katika shule hizo hulazimika kwenda mjini Longido na wengine hadi
Arusha mjini kuomba chakula kwa wasamaria wema ili waweze kupeleka nyumbani kwa
ajili ya mlo wa familia.
Kwa mujibu wa Sera ya Lishe Bora nchini Tanzania ya Mwaka 1992
lishe ni mchakato wa chakula mwilini na kila mwanadamu anapaswa kuzingatia makundi matano ya chakula ya nafaka,
matunda, mbogamboga, nyama na mafuta ili kuepukana na utapiamlo.
Wadau wa elimu mkoani Arusha wanashauri kwamba ili mwanafunzi aweze kusoma na kufaulu vizuri ni
lazima asiwe na changamoto ya njaa kwani pia upatikanaji wa lishe bora na
salama kwa matumizi ya wanadamu ni moja ya huduma za lazima kwa maisha na
ustawi wa wanadamu.
Katibu wa Jumuiya ya Wamiliki wa Shule na Vyuo Binafsi mkoani
Arusha (TAMNGOSE) Malias Mollel anakiri kuwa njaa inaweza kusababisha utoro kwa
wanafunzi na kusababisha ufaulu mdogo na kusisitiza kuwepo utaraibu wa upatikanaji
wa chakula cha mchana shuleni ambao utasaidia kuondoa tatizo la utoro kwa
wanafunzi.
Afisa Elimu Msingi Wilaya ya Longido, Deusdedit Bimbalirwa amekiri kumekuwepo na utoro katika shule za msingi kutokana na tatizo la njaa.
Bimbalirwa alisema kuna baadhi ya wanafunzi wameondoka na wazazi wao kwenda kutafuta malisho ya mifugo.
" Kwa kawaida
ukame unapokuwa mkali jamii za wafugaji huhama na mifugo sasa na wanafunzi
wanahama nao," alisema.
Alieleza kuwa pia
kutokana na njaa wanafunzi wanapungua madarasani na kurudi majumbani.
Anasema Halmashauri ya
Longido imeanza kulifanyiakazi tatizo hilo kwa kupeleka mashuleni na vijijini
chakula cha msaada na bei nafuu.
"Tayari chakula cha msaada kimeanza kupelekwa mashuleni lakini pia chakula cha bei nafuu ili kukabiliana na hali hii" alisema
Mahindi ya bei nafuu yaliyopelekwa na serikali
yanauzwa kwa shilingi elfu themanini (80,000/=)
kwa gunia. Hata hivyo, wananchi wanashindwa kununua
kwa sababu ya kipato duni kwani masharti ya serikali ni kuuza kwa gunia na siyo
kwa debe moja.
Bei ya mahindi katika soko la Longido ni shilingi 135,000 kwa
gunia na bei ya debe moja la mahindi linauzwa kati ya shilingi 24000/= mpaka
30000/= ambapo kama serikali ingeuza mahindi yake kwa debe moja wangeuza kwa
shilingi 16,000/=
Kutokana na uhaba
wa chakula unaokabili familia nyingi wilayani hapa, baadhi ya mashirika yasiyo
ya kiserikali yanayotekeleza miradi kudhibiti athari za mabadiliko ya tabianchi
katika wilaya hii ya Longido yameanza kusambaza chakula cha bure kwa kaya
zilizokumbwa na njaa.
Shirika la Utafiti,
Maendeleo na Huduma kwa Jamii (CORDS) limekabidhi tani 7.1 za mahindi kwa kaya
395 za vijiji viwili vya Ildonyo na Orpukeli ambapo kaya 165 za kijiji
cha Ildonyo zilipatiwa msaada wa chakula hicho na kijiji cha Orpukeli kaya 230
ambapo kila kaya ilipatiwa kg 20 za mahindi ili
kukabiliana na uhaba wa chakula.
Akizungumza wakati wa
ugawaji mahindi hayo, afisa idara ya miradi ya shirika la CORDS, Charles
Dominick alisema wameamua kutoa mahindi ya msaada baada ya kubaini kaya nyingi
zinakabiliwa na njaa kali kiasi kwamba watoto wanashindwa kwenda shule.
Kaimu Afisa Kilimo wa
wilaya ya Longido, Mariam Fivawo anasema ukame umesabisha uhaba wa chakula
katika maeneo mengi ya wilaya hiyo ambayo asilimia 95 ya wananchi wake ni
wafugaji.
No comments:
Post a Comment