SIMANJIRO WAMPOKEA KWA KUMTANDIKIA KANGA NAIBU WAZIRI WA AFYA - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Thursday, 13 July 2023

SIMANJIRO WAMPOKEA KWA KUMTANDIKIA KANGA NAIBU WAZIRI WA AFYA






Na Mwandishi wetu, Simanjiro. 


WAKAZI wa Kijiji cha Nakweni Kata ya Shambarai Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, wamempokea kwa kumtandikia kanga Naibu Waziri wa Afya Dk Godwin Mollel, wakati akiwakabidhi zahanati iliyojengwa na taasisi za dini.


Kijiji cha Nakweni kina wakazi 8,952 na pindi mtu akiugua na kutaka matibabu hulazimika kwenda kutibiwa kwenye kituo cha afya Mirerani kilichopo umbali wa kilomita 12.


Dk Mollel amezishukuru taasisi za dini zilizoshiriki kufanikisha, kujenga na  kukabidhi zahanati hiyo kwa serikali ili itumiwe na wakazi wa kijiji cha Nakweni.


"Baba Askofu Israel Gabriel Ole Maasa nawashukuru mno kwa niaba ya serikali kwa kufanikisha ujenzi wa zahanati hii itakayokuwa msaada mkubwa kwa jamii ya eneo hili," amesema Dk Mollel.


Amewashukuru wakazi wa kijiji hicho kwa mapokezi mazuri kwao kwa kutandika kanga barabarani ili wapite juu yake hivyo kuonyesha shauku na furaha ya kupokea zahanati hiyo.


Katibu mkuu wa jumuiya ya maridhiano Tanzania, Askofu wa kanisa la International Evangelisim  Dk Israel Ole Maasa, ambaye ni mkurugenzi wa shirika la All for his Glory wameshirikiana kujenga zahanati hiyo yenye vyumba 15.


Askofu Dk Ole Maasa amesema pamoja na zahanati hiyo pia wamechimba visima virefu vitatu kwa ajili ya wakazi wa kijiji hicho ambao ni wafugaji na wakulima.


Mkuu wa wilaya ya Simanjiro, Dk Suleiman Serera, amesema watumishi wawili, daktari na muuguzi wameandaliwa kuanza kazi pindi jengo hilo likikamilika.


"Mganga mkuu wa halmashauri ya Simanjiro (DMO) Dk Aristidy Raphael ambaye najivunia mno uchapakazi wake ameshawaandaa watumishi wawili kuanza kazi kwenye hii zahanati," amesema Dk Serera.


Ofisa mtendaji wa kijiji hicho, Noel Mollel amesema nguvu za wananchi zimetumika kwenye ujenzi wa vyumba nane hadi linta kwenye zahanati hiyo ni Sh10 milioni.


Mkazi wa kijiji hicho, Naishok Zephania amesema changamoto ya wagonjwa na wanawake wajawazito kufuata huduma za afya umbali mrefu zimefika ukingoni pindi zahanati hiyo ikianza kazi.



No comments: