![]() |
| Waziri wa Maliasili na Utalii Mheshimiwa Mohamed Mchengerwa |
Na: Mwandishi wetu,Arusha
maipacarusha20@gmail.com
Waziri wa Maliasili na Utalii, Mohamed Mchengerwa amezindua Kamati ya Ushauri ya Ugawaji wa Vitalu vya Uwindaji wa Kitalii nchini na kuipa majukumu kurekebisha kasoro zote zilizojitokeza katika sekta hiyo.
Sekta ya Uwindaji wa Kitalii ambayo ilikuwa imefifia Sasa imeanza kuimarika na mapato kwa mwaka yamefikia bilioni 30 na Sasa yanatakiwa kuongezeka zaidi.
Waziri Mchengerwa akizungumza baada ya kuunda kamati hiyo kwa mamlaka aliyopewa kwa mujibu wa kifungu cha 38 (1) na (2) ya Sheria ya Uhifadhi wa Wanyamapori sura ya 283 pia amesisitiza Uadilifu na weledi katika Utendaji kazi
Waziri Mchengerwa ameitaka Kamati hiyo kuondoa changamoto zote ili tasnia ijiendeshe kibiashara na kupunguza urasimu na mikinzano isiyokuwa na tija kwa Taifa.
“Ni imani yangu kwamba, kwa kuzingatia ushauri utakaotolewa na Kamati hii tasnia ya Uwindaji wa Kitalii itazidi kuimarika na kuvutia wawekezaji wa ndani na nje ya Nchi"alisema
Mchengerwa ambaye pia tangu kuongoza Wizara kumekuwepo na maboresho makubwa ya Utendaji na kuongeza mapato alisema kamati inapaswa kuhakikisha vitalu vyote vinapata wawekezaji ili kuongezea mapato ya Serikali ikiwa ni pamoja na vitalu 43 ambavyo kwa sasa vipo wazi.
Alisema anatarajia Kamati hiyo itafanya kazi kwa ufanisi na weledi katika utendaji kwa kuzingatia kuwa imesheheni wataalamu kutoka katika nyanja mbalimbali.
Amefafanua kuwa uwindaji wa kitalii unachangia katika pato la Taifa hususani fedha za kigeni na kwamba kwa wastani, Serikali inakusanya takriban shilingi Bilioni 30 kwa mwaka kutokana na Uwindaji wa huo na unachangia ajira za rasmi na zisizo rasmi kwa jamii.
Alisema kiasi hicho ni kidogo ukilinganisha na utajiri wa raslimali za wanyamapori hapa nchini ambapo ameitaka Kamati hiyo kufanya kazi na kujiwekea malengo makubwa zaidi.
Ameitaka Kamati hiyo kuzitambua changamoto zinazokabili tasnia hiyo ili kuja na mikakati ambayo itasaidia kuboresha sekta hiyo.
Amezitaja baadhi ya changamoto hizo kuwa ni pamoja na mabadiliko ya Sera na Sheria za Mataifa yanayoleta watalii wengi wa uwindaji, mabadiliko ya tabia nchi,uvamizi wa mifugo katika vitalu vya uwindaji wa kitalii hivyo kuathiri ustawi wa tasnia hii, na kampeni za wapingaji wa uwindaji wa kitalii ambazo kwa kiasi kikubwa zimeingilia maamuzi ya Mkataba wa Kimataifa unaosimamia Biashara ya Wanyamapori na Mimea iliyopo Hatarini kutoweka (CITES).
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Ushauri wa Ugawaji Vitalu
Profesa Jafary Kideghesho, amemhakikishia Waziri Mchengerwa kuwa Kamati yake itafanya kazi kwa weledi ili kufikia maono na Serikali ya kutaka tasnia hiyo kuchangia katia uchumi.
Naye Katibu wa Kamati hiyo ambaye pia ni Kamishna wa Mamlaka ya Wanyamapori nchini (TAWA) Mabula Nyanda amemshukuru Mhe. Mchengerwa kwa kuiunda Kamati hiyo ambapo amesema itasaidia kuboresha tasnia hiyo kwa kuwa imejumuisha wataalaam waliobobea katika tasnia hiyo.
Mara baada ya uzinduzi huo waziri Mchengerwa ametoa nyaraka na miongozo mbalimbali kwa wajumbe wote ikiwa ni namna ya kuwakabidhi nyenzo kwa ajili ya utekelezaji wa kazi zao.
Uwindaji wa Kitalii ni miongoni wa Idara ambazo zimekuwa nyeti kwa Wizara hiyo na watendaji kadhaa wamekuwa wakiingia katika migogoro kutokana na maamuzi Yao katika sekta hiyo.
Ili kupunguza migogoro Wizara hiyo ilianzishwa mfumo wa kugawa vitalu kutokana na mnada wa kielekroniki ambao hata hivyo bado unachangamoto .





No comments:
Post a Comment