LINDI WATAKIWA KUCHANGAMKIA FURSA ZA KIUCHUMI - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Sunday 27 August 2023

LINDI WATAKIWA KUCHANGAMKIA FURSA ZA KIUCHUMI

 



Na Mwandishi wetu, Ruangwa


maipacarusha20@gmail.com


WAZIRI Mkuu wa Kassim Majaliwa amewataka wakazi wa Mkoa wa Lindi kujihusisha na kujiingiza katika fursa za kiuchumi zilizopo hususan kwenye madini na siyo kuangalia kwa macho na kuwaachia wengine peke yao wafaidike na fursa hiyo.


Waziri Mkuu Majaliwa ameyasema katika viwanja vya Kilimahewa mjini Ruangwa mkoani Lindi kwenye maonesho ya madini na fursa za uwekezaji yenye lengo la kutangaza fursa za uwekezaji katika sekta ya madini na utalii.


Amesema watu wa Ruangwa na Lindi kwa ujumla wanapaswa kuchangamkia fursa za kuwepo madini mbalimbali na kujiingiza nao ili wasibaki kutazama fursa zikiwapita.


"Tusibakie kuangalia kwa macho fursa mbalimbali zikitupita nasi tujiunge ili tuweze kujinufaisha kiuchumi tukishirikiana na wadau tofauti wa maendeleo wanaotoka shemu tofauti nchini," amesema Waziri Mkuu Majaliwa.


Pia, amewaagiza wazalishaji wa madini ya chumvi nchini kuzalisha kwa wingi na kwa ubora ili kukidhi viwango vinavyohitajika katika soko la ndani na nje.


Ameitaka taasisi ya jiolojia na utafiti wa Madini Tanzania (GST) kuendelea kufanya tafiti mbalimbali za madini ili kugundua maeneo mapya ya uchimbaji madini kwa lengo la kuongeza wigo na fursa za ajira kwa watanzania.


Hata hivyo, amesisitiza uongezaji thamani madini kufanyika nchini kwa lengo la kuzalisha bidhaa zenye ubora zinatokana na madini na kuongeza ajira kwa watanzania  hivyo kuvutia wawekezaji wa ndani na nje ya nchi.


Pia, Waziri Mkuu Majaliwa ameziagiza halmashauri zote nchini kuandaa mpango wa uchimbaji endelevu, salama na utunzaji wa mazingira.

  

Rais mstaafu wa awamu ya nne Jakaya Kikwete ameipongeza Serikali kwa kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji na kuwataka wananchi wa Mkoa wa Lindi hususan Wilaya ya Ruangwa kutunza rasilimali zilizopo Mkoani humo ikiwemo ardhi.


"Mwaka 1988 nilikuwa Karibu wa CCM wilaya ya Nachingwea napafahamu huku hivyo nametoa wito kwa wananchi wa Lindi kuchangamkia fursa za uwekezaji zilizopo katika sekta ya madin," amesema Kikwete.


Waziri wa Madini Dotto Biteko amemshukuru Waziri Mkuu Majaliwa kwa kukubali kuwa mgeni rasmi katika kilele cha maonesho hayo ambapo amesema Wizara ya Madini itaendelea kusikiliza maelekezo yanayotolewa na viongozi ili kuipeleka sekta ya madini mbele.


Biteko amesema sekta ya madini inaongoza kwa kuliingizia Taifa fedha za kigeni kutokana na kuuza bidhaa za Madini.


Mkurugezi wa shirika la madini la Taifa (Stamico) Venance Mwasse amesema wanaendelea kutoa elimu kwa wachimbaji wa chumvi ili waandae kwa ubora waweze kupata soko zuri .


No comments: