Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Bima ya Taifa Bernard Konga akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha mapema leo. |
Na Andrea Ngobole, Arusha
maipacarusha20@gmail.com
MFUKO wa Taifa wa Bima ya afya Nchini (NHIF) umempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kusaini Sheria ya Bima ya Afya kwa wote kwani utasaidia kutoa matibabu kwa wote hususani kaya Maskini.
Sheria hiyo sasa itapelekea Wananchi wote kuwa na Bima itakayowawezesha kupata matibabu kwa wakati mijini na vijijini.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Samia Suluhu Hassan amesaini Sheria ya Bima ya Afya kwa wote ambapo kila Mtanzania Sasa atalazimika kupata Bima ili aweze kupata Matibabu
Mfuko wa BIMA ya Afya ya Taifa wapo jijini Arusha katika kutoa elimu kwa wadau wa Afya nchini, kutokana na maboresho ya Mfuko huo hasa katika kipindi hiki ambacho Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amesaini Sheria mpya ya Bima ya Afya kwa wote.
Bernard Konga ni Mkurugenzi Mkuu wa mfuko wa Bima ya Afya amesema wamekutana mkoani Arusha kwa lengo la kutoa Elimu ya Mfuko huo Kwa wadau wa Afya kutokana na Maboresho yaliyopo NHIF na kueleza uanzaji rasmi wa vifurushi vipya baada ya kusainiwa sheria ya bima ya Afya kwa Wote.
" Tumekuwa tukitoa Elimu Kwa mikoa Mbalimbali nchini na tupo kwenye Mwendelezo wa zoezi hili hapa mkoani Arusha hasa ukizingatia Sheria imesainiwa juzi na Mheshimiwa Rais hivyo kazi yetu Sasa kama Mfuko ni kutoa elimu Kwa wadau wa afya kuanzia Kwa watoa huduma, waajiri, wanachama na wananchi Kwa ujumla Ili kuelewa maboresho ya Mfuko na vifurushi vya Bima kwa sasa" alisema Konga.
Amesema kuwa vifurushi vipya vya Bima havitaathiri wateja walio na vifurushi vya zamani Kwa kuwa utaratibu umeandaliwa vizuri kuwa wale ambao tayari wana vifurushi wataendelea navyo hadi vitakapoisha ndipo wataanza kutumia vipya.
Meneja wa Bima ya Afya ya Taifa Mkoa wa Arusha Isaya Shekifu akifafanua jambo kwa wanahabari mapema leo |
Naye Meneja wa Bima ya afya Mkoa wa Arusha Isaya Shekifu alisema kwa sheria mpya kupita wananchi watapata huduma sawa ambapo hakutakuwa na utofauti mkubwa katika huduma za Matibabu huku akidai kuwa wanachama zaidi ya milioni 20 wanatarajiwa kuingia katika mpango wa Bima kutokana na kuwa serikali imetoa Fedha kwa ajili ya kaya milioni 15 ambazo ni Maskini Ili ziweze kupata bima ya Afya.
"Tutakuwa na skimu mbili ambayo Moja wapo ni skimu ya Watumishi wa Umma na skimu ya pili ni ya binafsi itakayoshughulika na sekta rasmi na zisizorasmi Kwa maana ya wananchi wote Kwa ujumla, na maboresho ni makubwa kutokana na Vituo na miundombinu kuboreshwa Kwa ajili ya kuhakikisha huduma zinatolewa ipasavyo"alisema Shekifu.
Alisema kwa sasa urasimu haupo kutokana na kila kitu kuendeshwa kilelekroniki hivyo kuondoa mtu wa kati ambaye anaweza kuwa kikwanzo na kila kitu kinakuwa kinaenda kwenye mfumo wa Serikali.
"Kulingana na maboresho Sasa Kila kitu kinaenda kimfumo zaidi na huduma zote zinazotolewa katika hosipitali Mbalimbali zitaonekana kwenye mfumo, Kwa maana ya aina ya ugonjwa na gharama zilizotumika na Matibabu aliyopatiwa mgonjwa vyote vinasomwa kwenye mfumo wa Serikali"alisema
No comments:
Post a Comment