MKAWE MABALOZI KATIKA KUELEZEA MAENDELEO YA WATOTO WENU- ASP NCHIMBI - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Thursday, 7 December 2023

MKAWE MABALOZI KATIKA KUELEZEA MAENDELEO YA WATOTO WENU- ASP NCHIMBI

 

Mkuu wa Polisi Jamii wilaya ya Monduli Mrakibu Msaidizi wa Polisi (ASP) Rashid Nchimbi akizungumza na wazazi pamoja na watoto wanohudumiwa na kituo cha Saint John Paul II Rehabilitation Centre kilichopo Monduli wakati Jeshi la Polisi lililopokwenda kutoa elimu juu ya Ukatili wa Kijinsia asubuhi ya leo

Mkuu wa Polisi Jamii wilaya ya Monduli Mrakibu Msaidizi wa Polisi (ASP) Rashid Nchimbi akiwa katika picha ya pamoja na watoto walemavu, wazazi na wafanyakazi wa kituo cha Saint John Paul II Rehabilitation Centre kilichopo wilaya ya Monduli mkoani Arusha

Baadhi ya wazazi wenye watoto walemavu wanaohudumiwa katika kituo cha Saint John Paul II Rehabilitation Centre pamoja na wafanyakazi wakipata elimu juu ya vitendo vya Ukatili iliyokuwa inatolewa na Jeshi la Polisi wilayani Monduli


Na Mwandishi Wetu, Monduli


maipacarusha20@gmail.com


Mkuu wa Polisi Jamii wilaya ya Monduli Mrakibu Msaidizi wa Polisi (ASP) Rashid Nchimbi, amewaomba wazazi waliowapeleka watoto wao wenye walemavu katika kituo kiitwacho Saint John Paul II Rehabilitation Centre kilichopo wilayani humo kwa ajili ya huduma mbalimbali wakawaeleze wenzao mafanikio waliyoyapata kutokana na maendeleo ya watoto wao.


ASP.Nchimbi aliyasema hayo kituoni hapo, baada ya Jeshi la Polisi kupata nafasi ya kutoa elimu ya Ukatili wa Kijinsia kwa wazazi wa watoto hao ambao wengi wao ni kutoka Jamii ya Kimasai.


Alisema kwa kuwa watoto wao wanapata matibabu, wanafanyiwa mazoezi, kupewa viungo bandia pamoja na elimu basi kwa mafanikio hayo wanatakiwa wafikishe taarifa hizo kwa ndugu, marafiki na majirani. 


" Endapo mtatoa taarifa za mafanikio haya kwa  wenzenu wenye matatizo  kama hayo, nao watapata muamko na hatimaye kuleta watoto wao kituoni hapa. Alisema ASP. Nchimbi.


Kwa upande wake mkuu wa Dawati la Jinsia na watoto wilaya ya Monduli , Mkaguzi Msaidizi wa Polisi Jacqueline Uhwelo, akiongea kituoni hapo ikiwa ni sehemu ya kampeni ya kupinga siku 16 za Ukatili wa watoto alisema kuwa, kumekuwa na matukio ya vipigo tena hadharani toka kwa akina baba kuwashambulia wenza wao lakini kutokana na mila potofu inasababisha wanawake hao kutotoa taarifa Polisi.


" Baadhi ya akina mama wa Jamii ya Kimasai wamekuwa wakifanyiwa vitendo vya Ukatili hasa vipigo lakini wakichinjiwa kondoo basi yanaisha, je mnadhani hizo mila potofu zitaisha lini? Alihoji Jacqueline Uhwelo ambaye ni Mkaguzi Msaidizi wa Polisi.


Naye Mratibu wa kituo hicho Bi. Mireile Kapilima pamoja na kulishukuru Jeshi la Polisi wilaya ya Monduli kwa kutoa elimu hiyo lakini pia akaahidi kuandaa kikao kikubwa kitakachowajumuisha wadau mbalimbali likiwemo Jeshi la Polisi kwa nia ya kuelimisha zaidi.


Kituo cha Saint John Paul II Rehabilitation Centre kimefanikiwa kuhudumia watu 12,000 toka kilipofunguliwa rasmi mwaka 1999.

No comments: