TAARIFA ZA MATOKEO YA SENSA YA WATU NA MAKAZI ZASAIDIA ZOEZI LA UHAKIKI WA WAATHIRIKA WA MAAFA HANANG - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Sunday 24 December 2023

TAARIFA ZA MATOKEO YA SENSA YA WATU NA MAKAZI ZASAIDIA ZOEZI LA UHAKIKI WA WAATHIRIKA WA MAAFA HANANG

 




Na Mwandishi wetu, Hannang


maipacarusha20@gmail.com


SERIKALI imetumia taarifa za matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi iliyofanyika mwaka 2022, kuthibitisha taarifa za makazi na kaya katika maeneo yaliyoathirika na maafa ya Maporomoko ya tope na mawe wilayani Hanang Mkoani Manyara.


Hayo yameelezwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera Bunge na Uratibu Mhe. Jenista Mhagama wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya matumizi ya matokeo ya sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022 kwa Viongozi na Watendaji wa Mkoa wa Ruvumatarehe 23 Disemba, 2023 .


Mafunzo hayo yaliyohusisha Kamati za Sensa na Wawakilishi wa Makundi Mbalimbali katika jamii, yakifanyika katika ukumbi wa Njunde– Halmashauri ya wilaya ya Songea Mkoani Ruvuma.


Waziri Mhagana amesema, moja ya jukumu muhimu walilonalo ni kupata taarifa ya hali ya kaya, makazi na mali katika maeneo yaliyoathirika kabla ya maafa hayo.


“Hitaji hili lilipelekea timu ya wataalamu kutoka Ofisi ya Taifa ya TAKWIMU kuja na taarifa ya kitaalamu iliyoambatana na picha za satellite ambazo zilionesha kwa uhakika hali ya kaya, makazi na mali zilizokuwepo katika maeneo hayo kwa idadi yake na maeneo zilizokuwepo,” amebainisha Waziri Mhagama.


Ameongezea kuwa,licha ya kwamba wametumia vyanzo vingine pia kuthibitisha baadhi ya masuala katika maeneo hayo, lakini chanzo cha kwanza cha kuaminika kimekuwa ni matokeo ya sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022.


Aidha ametumia fursa hiyo kuwakumbusha kuhusu maandalizi ya Dira ya Taifa ya Mwaka 2050 ambapo serikali imetoa fursa kwa wananchi kutoa maoni na mapendekezo.


”Niwasihi sana viongozi, watendaji na wananchi wote mshiriki katika zoezi hili ambalo ni muhimu kwa mustakabali mwema wa maendeleo ya nchi yetu, moja ya nyenzo muhimu zinazoweza kutuongoza kutoa maoni yetu ipasavyo historia ya taifa letu katika nyanja zote za siasa, uchumi, jamii pamoja na kuzingatia takwimu zinazozalishwa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu ikiwemo ya matokeo ya sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022,”amefafanua.


Kwa upande wake Mwantumu Athumani Meneja Takwimu Mkoa wa Ruvuma akizungumza kwa niaba ya Mtwakwimu Mkuu wa serikali, amesema utoaji wa matokeo ya sensa ni tofauti na matukio mengine ya kitakwimu kwa kuwa wigo wa sensa ni mpana zaidi.


”Matokeo ya sensa hutolewa kwa awamu kulingana na ratiba ya utoaji na usambazaji wa matoke hayo ,” amesema


Ameongeza kusema kama kuna mdau anahitaji matokeo ya sensa, ambayo hayapo kwenye ripoti zetu kwa sasa anakaribishwa kuleta maombi yake kwenye ofisi Takwimu za mikoa.


Naye Mkazi wa Peramiho Bw. Tito Sowela amesema elimu ya sensa ya watu na makazi imeongeza uelewa mpana wa wananchi hasa juu ya taarifa zinazokusanywa na namna zinavyoweza kusaidia serikali katika kupanga miradi ya maendeleo kwa wananchi.



No comments: