HALMASHAURI YA KIBAHA WAPOKEA GARI LA WAGONJWA, KUONDOA KERO KWA WANANCHI - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Monday 29 January 2024

HALMASHAURI YA KIBAHA WAPOKEA GARI LA WAGONJWA, KUONDOA KERO KWA WANANCHI

 




Na Mwandishi wetu


maipacarusha20@gmail.com


HALMASHAURI ya Wilaya ya Kibaha imepokea gari ya wagonjwa ambayo itatumika katika Hospitali ya Wilaya hiyo na kuondoa kero iliyokuwepo awali iliyosababishwa na uhaba wa magari hayo.


Akikabidhi gari hilo  kwa Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Mbunge wa Jimbo la Kibaha Vijijini Michael Mwakamo alitoa tahadhari katika matumizi ya gari hilo kutumika kama daladala ya kubebea watendaji.


Mwakamo alisema Ili gari hilo lidumu kwa muda mrefu linatakiwa kutumika kwa malengo yaliyokusudiwa  lisiharibike mapema.


"Gari hili linakuja kuondoa kikwazo Cha uhaba wa magari kilichokuwepo awali, natoa angalizo lisitumike kama daladala ya kubebea watendaji wanapoenda kazini, pandeni daladala, bajaji sio kupanda kwenye hili gari mkifanya hivyo tatizo litarudi tena," alisisitiza.


Mwakamo alijivunia jitihada zake za kuleta maendeleo katika Jimbo hilo huku akiishukuru Serikali kwa namna inavyotoa fedha na vitendea kazi kumaliza kero za Wananchi.


Mganga Mkuu wa Halmashauri hiyo Dk.Wilford Kondo alisema kwamba hakuna mgonjwa atakayetozwa fedha kwa huduma ya gari hilo la wagonjwa na kwamba atakayedaiwa fedha ya mafuta atoe taarifa.


Kadhalika Dk Kondo aliwataka Wananchi kufika kupata huduma katika Hospitali ya Wilaya kwani huduma nyingi kwasasa zinapatikana katika Hospitali hiyo tofauti na awali ambapo ilikuwa lazima mgonjwa apewe rufaa kwenda Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Pwani Tumbi.


Diwani wa Mlandizi Euphrasia Kadala akiishukuru Serikali kwa kutoa gari hilo la wagonjwa kwa ajili ya Hospitali ya Wilaya  ambalo sasa litakwenda kuondoa adha ya kukodi magari pindi lililopo linapopata hitilafu.


Tatu Haji na John Pilly ni wakazi wa Mlandizi ambao wanaishukuru Serikali kwa ajili ya gari hilo litakalosaidia kuhudumia wagonjwa kwa haraka.



No comments: