AWESO AZITAKA JUMUIYA ZA MAJI KUPELEKA FEDHA BENKI ILI MIRADI IWE ENDELEVU - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Monday 29 January 2024

AWESO AZITAKA JUMUIYA ZA MAJI KUPELEKA FEDHA BENKI ILI MIRADI IWE ENDELEVU

 

Waziri wa Maji Juma Aweso akizungumza na wakazi wa kata ya Chumbi  Wilayani Rufiji

Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakari Kunenge akimtwisha ndogo ya Maji Mkazi wa kata ya Chumbi Wilayani Rufiji 



Na; Mwandishi wetu


maipacarusha20@gmail.com


WAZIRI wa Maji Jumaa Aweso amesema Jumuiya za maji zinatakiwa kuzingatia utaratibu wa kupeleka fedha benki ambao utasaidia miradi hiyo kuwa endelevu.


Aweso ameyasema hayo alipokuwa akizindua mradi wa maji katika kata ya Chumbi Wilaya ya Rufiji Mkoani Pwani uliojengwa kwa usimamizi wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) kwa gharama ya sh. miln 722.


Alitoa maelekezo kwa Jumuiya za watumiaji maji ambao wanasimamia mradi huo wa Chumbi kuhakikisha fedha wanazokusanya zinawekwa benki Ili mradi uwe endelevu.


Anasema amekuwa akishuhudia baadhi ya Jumuiya wananchi wanakusanya fedha baadae viongozi wao wanagawana kwa kupokezana na inapotokea mmoja wa wajumbe kukosa huanzisha ugomvi unaosababisha kuvunjika Jumuiya.


"Nataka niwaambie vipo vya kuchezea ukishiba chezea kidevu chako sio fedha za miradi ya maji tutashighulikiana,".


Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge ameishukuru Serikali kwa kutoa fedha za kutekeleza miradi mbalimbali inayotatua kero za Wananchi.


Kunenge amesema mradi huo unakwenda kuondoa kero ya wananchi kutumia muda mwingi kusaka maji.


Mradi wa maji Chumbi ambao umeanza kutumika unatarajia kuhudumia zaidi ya wakazi 8000 wa Vijiji vya Chumbi A, B, na C.


"Niwaombe sana mradi huu umekamilika leo mnapata maji safi na salama faida yake mama ambaye alikuwa anatembea umbali mrefu leo atayapata maji karibu na kama kulikuwa na mlipuko wa magonjwa sasa watu watakuwa salama,".


Pia alitoa Ombi kwa wananchi hao kutunza mradi huo kwani kumekuwa na shuhuda kwa baadhi ya maeneo Serikali kujenga miradi na baadae baadhi yao kuiharibu na kurudisha kero iliyokuwepo awali


Katika hatua nyingine Waziri Aweso alimuagiza Meneja RUWASA mkoa wa Pwani Beatrice Kasimbazi pamoja na Meneja wa Wilaya ya Rufiji kutumia fedha walizonazo kwenye akaunti zao kufikisha maji katika kitongoji cha Nyakipande.


Kitongoji Cha Nyakipande ni kati ya vitongoji vya Kata ya Chumbi kikiwemo Chumbi A, B, na C na ndicho pekee hakijafikiwa na huduma hiyo ya maji.


Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge alisema mradi huo ni kati ya miradi inayotatua kero za Wananchi.


Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Rufiji ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga Hadija Nasr alimuomba Waziri Aweso kuangalia namna ya kuanzisha mamlaka za maji katika mkoa huo Ili kuimarisha huduma.


Mmoja wa wananchi wa Chumbi Asha Pondamali akiishukuru Serikali kwa mradi huo ambapo alisema awali iliwalazimu kulala visimani wakisubiri maji .


Asha alisema kuna wakati wanawake walijifungulia kisimani wakisumlbiri maji kutokana na adha waliyokuwa nayo na sasa mradi huo utakwenda kuwawezesha kufanya shughuli za maendeleo na kulinda ndoa zao.



No comments: