NAIBU WAZIRI KATAMBI APONGEZA HALI YA UTOAJI HUDUMA KITUO CHA OSBP NAMANGA - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Thursday 4 January 2024

NAIBU WAZIRI KATAMBI APONGEZA HALI YA UTOAJI HUDUMA KITUO CHA OSBP NAMANGA

 




Na Elinipa Lupembe, Arusha


maipacarusha20@gmail.com


Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana na Wenye Ulemavu Mhe. Pascal Katambi Patrobass (Mb), amepongeza hali ya utoaji na upatikanaji wa huduma  kwa wasafiri wanaopitia mpaka wa Tanzania na Kenya kupitia Kituo cha Huduma za pamoja Mpakani (OSBP), eneo la Namanga.


Mhe. Katambi amesema hayo wakati alipofanya ziara ya siku moja ya kukagua hali halisi ya utendaji kazi na utoaji huduma katika mpaka huo kwa wasafiri, mali na mizigo yao pamoja na magari ya mizigo na kupongeza namna Serikali imeweka mifumo rahisi ya kudhibiti upitaji wa abiria na mizigo.


Amesema kuwa, licha ya Kituo cha pamoja kuwa na mifumo inayowarahisishia abiria kupita mpakani, amewataka wataalam kuzingatia hali ya usalama katika mipaka kwa kufanya upekuzi wa abiria na mizigo yao pamoja na magari ya mizigo kwa umakini na kujiridhisha.


"Uwepo wa miundombinu rafiki yenye mifumo ya kisasa, unaruhusu kila abiria kukaguliwa na kulipia na kupata vibali vyote katika eneo moja pamoja na kudhibiti usafirishaji haramu wa mali na binadamu, kituo ambacho kina hadhi ya kimataifa" 


Naye Mfawidhi wa Uhamiaji mpaka wa Namanga, Mrakibu wa Uhamiaji Bulugu Edward Mkanga, amesema kuwa makubaliano ya 'communique' yanayoruhusu raia wa nchi hizo mbili kutembea hadi Km 20 kwa pande zote umepunguza uhalifu na kuongeza muingiliano wa kibiashara katika eneo la Tanzania.


Raia wa Kenya anaruhusiwa kuingia hadi kipenyo cha Km 20 katika eneo la Tanzania kadhalika na raia wa Tanzania anaruhusiwa kuingi Kenya, jambo ambalo limefanikiwa kuongeza muingiliano wa kibiashara mpakani huku Tanzania ikinufaika kutoka na wakenya kupenda kufika Tanzania.


Hata hivyo, Mkuu wa wilaya ya Longido, Mhe. Marco Ng'umbi, amesema kuwa hali ya usalama wilayani hapo ni shwari huku wakazi wake wakiendelea na shughuli zao za kila siku za kujitafutia kapato.


"Wilaya ya Longido inaendelea kuunga mkono juhudi za Serikali ya awamu ya sita, inayoongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kusimamia matumizi ya mifumo inayotumika kwenye kituo cha Huduma za Pamoja Mpakani (OSBP) Namanga, na kuhakikisha raia wanaoingia na kutoka nchini wanafuata taratibu zote, huku kukiwa na utaraibu mzuri wa ukaguzi wa magari madogo na magari ya mzigo kabla ya kuvuka na kuingia nchini" Amefafanua Mhe. Ng'umbi


#arushafursalukuki🇹🇿







No comments: