Waziri Jerry Slaa Atoa Siku 30 Kumalizwa Mgogoro wa Ardhi Jijini Arusha. - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Monday 29 January 2024

Waziri Jerry Slaa Atoa Siku 30 Kumalizwa Mgogoro wa Ardhi Jijini Arusha.



waziri wa Ardhi Nymba na Makazi Jerry Slaa


Na: Andrea Ngobole, Arusha

maipacarusha20@gmail.com

Kamishna wa ardhi mkoa Arusha, amezuia zoezi la utolewaji hati za umiliki wa ardhi, katika eneo la ekari sita, lililopo kata ya Olmoti katika jiji la Arusha kutokana na eneo hilo kuwa na mgogoro kwa miaka 17 sasa, ili kutekeleza agizo la waziri wa Ardhi Jerry Slaa aliyetoa siku 30 kumalizwa mgogoro huo.


Waziri wa ardhi,Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Slaa wiki iliyopita, alitembelea eneo hilo na kuzungumza na William Mollel ambaye analalamika eneo lake kuvamiwa pamoja na majirani wa eneo.


Katika mgogoro huo, Familia ya Mollel inamtuhumu aliyekuwa Afisa Ardhi jiji la Arusha, Chritopher Kitundu ambaye hivi sasa amehamishiwa wilaya ya Tandahimba kuuziwa eneo na Leah Neeva hilo kinyume cha sheria na kuanza kuuza viwanja.


Hata hivyo, Kitundu alikana kuvamia eneo hilo na kueleza wanaomlalamikia waende mahakamani badala ya kumtuhumu kuvamia eneo lao.


"Mimi sijavamia eneo la mtu, kama kuna wanaonilalamikia basi waende mahakamani "alisema


Akizungumza katika kikao cha kutafuta suhulu ya mgogoro huo, Kamishna Mwamsojo akiwa na Afisa ardhi wa mkoa Arusha, Neema Ulomi juzi, alieleza ameamua kusitisha utoaji hati wa viwanja katika eneo hilo, hadi suluhu itakapopatikana.


Alisema katika kutekeleza maagizo ya Waziri, Slaa leo jumatatu January 29 akiwa na maafisa wake, watafika tena katika shamba lenye mgogoro na kuzungumza na pande zote lakini pia na majirani ambao nao wanalalamika kumegwa ardhi yao.


"Tumepata taarifa kupimwa kwa eneo hilo na maafisa wetu wa ardhi licha ya kuwepo mgogoro na kuanza kuuzwa viwanja taratibu za kinidhamu zinaendelea na sasa tumetisitisha utoaji wa hati"alisema


Awali Mollel alisema kwa miaka 17 wamekuwa katika mgogoro huo, baada ya Neeva Savoroi ambaye alivamia shamba hilo ambaye tayari alifariki na baadaye mkewe Leah Neeva kuendelea kulimiliki kinyume cha sheria na kumuuzia Kitundu.


Alisema suala hilo tayari lilifikishwa baraza la ardhi la Kata kwa shauri namba S/2006 ambalo alishinda na baadaye shauri kuhamishiwa baraza la ardhi wilaya na baada ya kukata rufaa mahakama ya rufaa, shauri hilo lilirejeshwa baraza la ardhi.


"Hata hivyo wakati shauri lipo bado katika baraza la ardhi,Kitundu alitumia maafisa wenzake wa ardhi, kwenda kupima eneo hilo na kukata viwanja ploti namba 60-70 Block A,Plan No E/248/205 mnano Agosti mwaka jana"alisema


Alisema baada ya tukio hilo, walipeleka malalamiko baraza la ardhi na ofisi za Serikali Kata ya Olmoti, ambao walifika shambani na kuagiza kusitishwa upimaji lakini maafisa hao walikaidi.


Mwenyekiti wa baraza la ardhi Kata ya Olmoti, Yusuph Abdalah alikiri kuwepo na shauri la mgogoro huo, hata hivyo, alisema mlalamikiwa aliyeuza eneo hilo, Leah Neeva ameandika barua kutokuwa na imani na baraza na hivyo hatashiriki katika shauri hilo.


"Hili shauri bado lipo hapa, kwetu lakini Mlalamikiwa amekuwa hafiki kwenye vikao vya baraza na tayari ameandika barua rasmi kutokuwa na imani na baraza la ardhi"alisema.


Hata hivyo,Neeva akizungumzia eneo hilo, ameeleza ni eneo la famia yake na waliuziwa na Mollel(ambaye analalamika kuvamiwa) miaka ya nyuma .

No comments: