BINTI AUWAWA BAADA YA KUKATAA KUOLEWA WILAYANI NGORONGORO - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Saturday 10 February 2024

BINTI AUWAWA BAADA YA KUKATAA KUOLEWA WILAYANI NGORONGORO





Na: Mwandishi wetu, Arusha 

maipacarusha20@gmail.com

Mtandao wa watetezi wa haki za watoto, wanawake na wasichana Taifa (TAPO) umelaani tukio la kupigwa na kuuawa kwa msichana wa jamii ya Kimasai akiwa na ujauzito ,Nanyoli Mohee baada ya kugoma kuolewa .


Akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha, mmoja ya viongozi wa mtandao huo Neema Laizer, alisema tukio hilo la kinyama limetokea mwanzoni mwa wiki hii katika kijiji cha Malambo wilayani Ngorongoro mkoa wa Arusha.



Alisema mwanaume wa jamii hiyo aliyemtaja kwa jina la Amyor Matayo alimshambulia msichana huyo mwenye umri chini ya miaka 16 kwa kumpiga na fimbo mbele ya baba yake mzazi akimlazimisha kumpeleka nyumbani kwake kama mke kwa kuwa alishamlipia mahali kwa wazazi wake wakati akiwa mtoto mdogo.



"Binti aligoma kuondoka kwenda kuolewa ndipo baba yake alimtaka mumewe amchape kwa fimbo"


Awali binti huyo alichukuliwa na mwanaume huyo kwa ajili ya maisha ya ndoa lakini alitoroka nyumbani kwa mwanaume huyo na kwenda kuishi porini, lakini alikuja kugunduliwa na mpita njia ambaye aliamua kumrejesha nyumbani kwa wazazi wake.



"Februali 6, mwaka huu mtu mmoja anayemfahamu alimkuta porini akiwa amedhoofu na kumkamata na kisha kumrejesha nyumbani kwa wazazi wake"


Laizer alisema Baba mzazi wa binti huyo aliamua kumpigia simu mwanaume huyo aliyekuwa akiishi kijiji cha Endepes wilayani humo na kumtaarifu kuwa mke wake alikuwa nyumbani kwake na aje kumchukua".



"Baada ya kufika mwanaume huyo alimtaka binti huyo waondoke lakini alikataa ndipo alipochukua fimbo na kuanza kumshambulia mbele ya baba yake na kumjeruhi vibaya maeneo mbalimbali ya mwili wake"


Alisema binti huyo alipiga kelele kutokana na maumivu aliyokuwa akiyapata na majirani walifika nyumbani kwa baba yake na kumkuta akiwa na hali mbaya na kuamua kumpeleka katika hospitali ya Malambo kwa ajili ya matibabu lakini siku iliyofuata alifariki dunia.


Naye Iddy Ninga kutoka Mtandao wa kupiga ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na watoto alisema wao kama TAPO wamesikitishwa na tukio hilo na kutoa tamko kuwa mwili wa marehemu usizikwe hadi hapo uchunguzi wa kina utakapofanyika na taarifa ya uchunguzi ikabidhiwe kwa vyombo husika vya sheria.
Iddy Ninga akifafanua jambo Kwa waandishi wa Habari jijini Arusha 



Pia wamevitaka vyombo vya ulinzi na usalama yakiwemo madawati ya kijinsia kutekeleza majukumu yake kikamilifu ili kuhakikisha haki inatendeka katika kushughulikia suala hilo na serikali ichukua hatua kali juu ya matukio ya aina hiyo yaliyokithiri kwa jamii za kifugaji.


Aidha wameitaka serikali ipeleke mswada kwa ajili ya mabadiliko ya kifungu cha 13 na 17 cha sheria ya ndoa ya mwaka 1971 inayoruhusu mtoto wa kike kuolewa akiwa na umri wa miaka 14 Kwa ridhaa ya wazazi wake.


 Rose Njilo Mkurugenzi wa Shirika la Mimutie women organization linalojihusisha na utetezi wa haki ya mtoto na wanawake katika jamii za pembezoni alisema matukio ya mabinti wenye umri mdogo kulazimishwa kuolewa yamekithiri kiasi kwamba yamekuwa yakisabahisha vifo.
Rose Njilo Mkurugenzi Mtendaji wa Mimutie Women Organization akieleza madhila wanayokutana nayo watoto wa kike wanaolazimishwa kutolewa nchini Tanzania 



Mkurugenzi huyo alitoa mfano kwa baadhi ya matukio ya watoto wa kike kufanyiwa ukatili wa kulazimishwa kuolewa ambayo aliripotiwa mwaka 2022 ni pamoja na tukio la Rebecca Benjamini mkazi wa kata ya Isunya , mkoa wa Geita ambapo binti huyo aliamua kujinyonga na kufa baada ya wazazi wake kumlazinisha kuolewa.



"Rebecca alifariki dunia kwa kujinyonga kwa kamba baada ya kukazimishwa kuolewa na kuachika mara tatu "


Alisema tukio jingine lilitokea katika kijiji cha Lufubu Mkoani Kigoma ambapo binti aliyefahamika kwa jina la Mbaru Juakali (17)alifariki dunia kwa kipigo cha baba yake mkùbwa baada ya kukataa kuolewa wakati wazazi wake wamepokea mahari ya ng'ombe 13.


Tapo wamedai kwamba watu wawili wanashikiliwa na jeshi la polisi wilayani humo ambao ni Mume wa marehemu pamoja na baba mzazi wa marehemu.


Aidha wameiomba serikali na wadau mbalimbali kushirikiana ili kutokomeza matukio ya ukatili dhidi ya watoto wa kike na kulitaka jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha kuchukua hatua za kisheria na wahusika kufikishwa mahakamani.

No comments: