Chuo Cha Mipango Chaanza Mkakati Maalumu Wa Kutoa Elimu Jumuishi - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Friday 2 February 2024

Chuo Cha Mipango Chaanza Mkakati Maalumu Wa Kutoa Elimu Jumuishi










Na Mwandishi wetu, Dodoma

maipacarusha20@gmail.com


TAASISI ya Chuo Cha Mipango ya Maendeleo Vijijini (IRDP) chenye makao yake makuu Jijini Dodoma kinatekeleza mradi maalumu wa kujenga mazingira wezeshi ya kujifunzia kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum ambao wamejiunga katika kituo hicho.

Mpango huo endelevu unaolenga kutoa elimu jumuishi unatekelezwa chini ya ufadhili wa mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET), pamoja na vyanzo vya ndani vya Taasisi hiyo.


Katika mahojiano maalum na MAIPAC Media Tanzania, Mkuu wa chuo cha IRDP, Profesa Hozen Mayaya alieleza kuwa taasisi hiyo inayofanya kazi chini ya Wizara ya Fedha imeamua kutekeleza mradi huo ili kuhakikisha wanafunzi wenye mahitaji maalum wanapata haki zao za kisheria za kupata elimu bora.

Ili kuhakikisha mradi unapata matokeo chanya, Prof Mayaya amesema taasisi ipo katika mchakato wa kuajiri waalimu wenye weledi wa kuwafundisha wanafunzi wenye mahitaji maalumu.

“Katika waraka wetu unaohusu utaratibu wa utumishi wa chuo, tumeomba kuajiri wataalamu mahiri kwa ajili ya kuwafundisha wanafunzi wenye mahitaji maalum, na tayari tumepeleka waraka huo kwenye Ofisi ya Rais, Manajimenti Ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa ajili ya kuhidhinishwa," Prof Mayaya alieleza.





Kupitia mradi huo, alieleza kuwa taasisi inafanya kazi ya kuwatambua wanafunzi wenye ulemavu wa aina mbalimbali ili kuwa katika nafasi nzuri ya kuwasaidia kulingana na aina za changamoto za kimwili walizonazo.

"Leongo ni kuhakikisha chuo kinakuwa sehemu bora na rafiki kwa makazi na kutoa elimu bora kwa wanafunzi wote walioandikishwa, bila kujali hali zao za kimwili," alielezea.

Akitoa maelezo zaidi kuhusu mradi huo, Dkt. Sagumo Malenda, Mratibu wa Elimu Jumuishi (EI) chini ya Mradi wa HEET katika taasisi hiyo, alieleza kuwa kwa sass chuo kina zaidi ya wanafunzi 27 wenye mahitaji maalumu.

Aidha, amesema idadi hiyo inajumuisha wale wenye ulemavu wa kusikia, aina tofauti za ulemavu wa viungo, uoni hafifu pamoja na ulemavu wa ngozi (albinism).

“Katika awamu ya kwanza, IRDP ilipokea takribani shilingi milioni saba kutoka kwa mradi wa HEET kwa ajili ya kuhudumia wanafunzi wenye mahitaji maalum, kiasi ambacho kilitumika kuendesha zoezi muhimu la kuwatambua, katika kampasi zote mbili za Mwanza na Dodoma, pamoja na kuwapatia misaada mbalimbali,” alieleza.

Aliongeza kuwa, pamoja na huduma nyingine, mradi unajikita kuwapatia wanafunzi hao vifaa mbalimbi vya kuwasaidia, pamoja na kuhakikisha chuo kinajenga miundombinu rafiki.

"Kwa mfano, mradi unalenga kuhakikisha hosteli za wanafunzi na madarasa yote yanawekwa miundombinu rafiki kwa ajili ya kusaidia wanafunzi wenye mahitaji maalum," alisisitiza.

Taasisi ya Mipango ya Maendeleo Vijijini (IRDP) ni chombo cha ushirika kilichoanzishwa kwa Sheria ya Bunge Na. 8 ya 1980.

No comments: