Na: Mwandishi wetu, Pwani
maipacarusha20@gmail.com
Mdau wa masuala ya kijamii, ambae pia ni mtunzi wa vitabu kutoka Mkoa wa Pwani, Rehema Kawambwa ametoa fulana alizozipa jina la "Pwani Tulivu" ambazo zina nembo inayoonesha picha yenye samaki, ngalawa, bahari, na minazi .
Nembo hiyo pia inaakisi vitu vinavyopatikana katika Mkoa wa Pwani, kwa lengo la kuunga mkono jitihada za Serikali katika kuuhamasisha, na kuutangaza uchumi wa bluu katika Mkoa huo.
Rehema anasema lengo ni kuutangaza Mkoa huo kuwa ni tulivu katika shughuli za uwekezaji, na amani imetawala hivyo watu wote wanakaribishwa kuvitembelea vivutio vya utalii vilivyopo, na kuja kujionea mambo yote mazuri yanayopatikana katika Mkoa huo.
Rehema ameeleza kwamba hilo ni toleo la nne tangu aanze kuchapisha fulana hizo kuhusiana na masuala ya utalii kupitia toleo lake la kwanza la mwaka 2021 alilolipa jina la Utalii Kisarawe, la pili la mwaka huo huo 2021 na la tatu la mwaka 2022 alilolitumia jina la Pwani Pazuri, na kutofautisha nembo, na sasa kujikita kuutangaza uchumi wa bluu uliopo mkoani hapo.
"Wakati Serikali ikiendelea kuhimiza uchumi wa bluu na kuvutia wawekezaji kuona umuhimu wa uwekezaji wa bahari na viwanda vya kuchakata samaki, mimi kama kijana nimeona nijielekeze kuchagiza, na kuchechemua jamii kuhusu uchumi wa bluu kwenye Mkoa huo," aliongeza Rehema.
Rehema ametoa rai kwa jamii kujali usafi, na utunzaji wa mazingira ya hifadhi za maeneo ya bahari na fukwe, pia kusimamia rasilimali zitokanazo na bahari ili kuhakikisha maendeleo endelevu, na kuvilinda viumbe vilivyo hatarini kutoweka.
Aidha, amewasihi wananchi kujiunga katika vikundi vya ushirika ili wawezeshwe na Serikali kunufaika na fursa zitokanazo katika uchumi wa bluu zikiwemo ufugaji wa samaki, na kilimo cha mwani.
Mkoa wa Pwani, una vivutio 82 vya utalii ikiongozwa na Mafia ambacho ni kitovu cha utalii katika Mkoa huo.
No comments:
Post a Comment