MAHAKAMA YA TANZANIA YAAMURU KULIPWA TSH 169,264,200/= KWA WAFUGAJI KUTOKANA NA MNADA USIO HALALI - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Wednesday 14 February 2024

MAHAKAMA YA TANZANIA YAAMURU KULIPWA TSH 169,264,200/= KWA WAFUGAJI KUTOKANA NA MNADA USIO HALALI

 


Baadhi ya Wafugaji wa tarafa ya Loliondo ambao mifugo ilitaifishwa




Na: Mwandishi wetu, MAIPAC 


maipacarusha20@gmail.com


Mahakama ya Hakimu Mkazi Musoma imetoa Amri ya kurudishiwa kiasi cha shilingi za Kitanzania 169,264,200/= kwa Bw. Oloomu Kursas, Sinjore Maitika na Ndagusa Koros kutokana na mauzo kwa  njia ya mnada usio halali wa mifugo ya wafugaji hao. 

Mahakama iliamuru kurudishwa kwa pesa hizo baada ya kubaini kuwa mnada uliofanyika tarehe 1 Novemba 2023 wa ng'ombe 806, kondoo 420 na mbuzi 100 mali za wafugaji hao kutoka Loliondo ulifanyika kinyume cha Sheria.

 Kesi hiyo ilisimamiwa kwa msaada wa mawakili kutoka Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC).


 Historia ya Kesi

Tarehe 26 Oktoba 2023, Ng'ombe wapatao 806, Kondoo 420 na Mbuzi 100 wa Bw. Oloomu Kursas, Sinjore Maitika na Ndagusa Koros walikamatwa na askari wa wanyamapori katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti. 

Mifugo hiyo ilidaiwa kukutwa eneo la Long'osa wilayani Serengeti, Mkoa wa Mara.

 Baada ya kukamatwa mifugo hiyo ilisalia katika Kituo cha Askari Wanyamapori cha Lobo ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.


Mnamo Tarehe 30 Oktoba 2023, Jamhuri ilifungua kesi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Musoma kuiomba mahakama hio kutoa amri ya kuuza mali hizo kwa njia ya Mnada (maombi ya upande mmoja Na. 10 ya 2023).

 Mawakili wa Serikali walidai kuwa mifugo hiyo haikubainika kuwa wamiliki wake ni wakina nani. Tarehe 31 Oktoba 2023, Mahakama hiyo ilitoa amri ya kuuza mifugo hio kwa njia ya mnada . 

Msimamizi wa mnada aliteuliwa kufanya mnada huo kwa kuzingatia sheria na taratibu zote za uendeshaji wa minada.


Mara tu baada ya Amri ya Mahakama, Bw. Oloomu Kursas, Sinjore Maitika na Ndagusa Koros walifungua maombi Mahakama Kuu ya Tanzania Masijala ya Musoma, wakiiomba Mahakama Kuu irekebishe Amri ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Musoma itamke kuwa mifugo hiyo ilikuwa ni mali yao wenyewe na kwani madai ya Jamhuri kuwa mali hizo zilikuwa hazijulikani mmiliki wake hayakuwa ya kweli. 

Hii ni katika (Maombi ya marekebisho Na. 08 ya 2023).


Bw. Oloomu na wenzake waliiambia pia Mahakama kuwa, hata kama mali hizo zingekuwa hazijulikani mmiliki wake, bado taratibu za kisheria hazikufuatwa ambazo zinataka mali ambazo mmiliki wake hajajulikana zitangazwe hadharani ili wamiliki waweze kujitokeza. 

Hii ni chini ya Kifungu cha 25 cha Sheria ya Hifadhi za Taifa na Kifungu cha 47 cha Sheria ya Jeshi la Polisi  na Huduma Saidizi.Tarehe 10 Novemba 2023, Mahakama Kuu ilitengua Uamuzi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi ikiamuru kesi hiyo kusikilizwa upya.


Wakati huohuo Bw. Oloomu, Maitika na Ndagusa walifungua maombi ya zuio wakiiomba Mahakama Kuu izuie kuuzwa kwa Mifugo hiyo kwa njia ya Mnada katika (Maombi Na. 35 ya 2023). 


Tarehe 1 Novemba 2023 Mahakama Kuu ilitoa Uamuzi ikisema kuwa uuzaji usitishwe kwa sababu Bw. Oloomu, Maitika na Ndagusa walinyimwa haki yao ya kusikilizwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Musoma. Hata hivyo, dalali wa Mahakama alitangaza mnada na kuuza Ng'ombe, kondoo, na mbuzi zote. Bw. Oloomu na wenzake waliieleza Mahakama Kuu kuwa uuzwaji wa mifugo hiyo haukufuata Sheria na taratibu za minada sababu walitangaza mnada Tarehe 1 Novemba 2023 na kuuza mifugo hiyo, siku hiyo hiyo.


Imetolewa na Idara ya Utetezi

Mtandao wa Watetezi Wa Haki za Binadamu Tanzania(THRDC)

Dar es Salaam, Tanzania.

14 Februari 2024.




No comments: