Mwendesha Mashitaka wa TAWA Getrude Kariongi akitoa mafunzo kwa askari wa wanyamapori |
Mwandishi wetu,Babati
maipacarusha20@gmail.com
Ofisi ya Mkurugenzi wa mashtaka Mkoa wa Manyara kwa kushirikiana na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori (TAWA) Kanda ya kaskazini ,imewasilisha notisi ya kukata rufaa, mahakama kuu kanda Manyara,kupinga kuachiwa huru ,watuhumiwa watatu wa ujangili, waliokamatwa na vipande sita vya meno ya Tembo.
Watuhumiwa hao,Bashiru Ally Nahai, Daniel Gwandu na Frank Gadiye,walikamatwa machi 3,mwaka jana, wakiwa na vipande sita vya meno ya tembo kinyume cha sheria vyenye thamani ya sh 137,910,300 eneo la njia panda ya Madunga,Kata ya Madunga, wilayani Babati,mkoa wa Manyara.
Watuhumiwa hao, walifikishwa mahakamani na kukabiliwa na makosa matatu ya uhujumu wa uchumi,ikiwepo kupanga njama za uhalifu,kukutwa na meno na Tembo na kamatwa wakisafirisha meno hayo kinyume cha sheria.
Mwendesha Mashtaka wa TAWA, Getrude Kariongi amesema wanakata rufaa kupinga kuachiwa huru watuhumiwa hao na mahakama ya mkoa Manyara katika hukumu iliyotolewa Novemba 20 mwaka jana.
"Baada ya kupokea nakala ya hukumu, tumeipitia na kuona tunasababu nyingi za msingi kukata rufaa, kwani upande wa mashitaka tulijiridhisha na ushahidi wa kutosha kwamba watuhumiwa hawa kuhusika na ujangili"amesema
Amesema Katika hukumu ya kesi ya uhujumu uchumi namba 4,2023 iliyosomwa na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Mkoa Manyara, Mariam Lusewa wameona hukumu inamapungufu hivyo wanaamini, mahakama kuu itaweza kutoa hukumu ya haki.
Katika hukumu hiyo, Hakimu Lusewa amesema upande wa mashitaka umeshindwa kuthibitisha pasi na shaka tuhuma za watuhumiwa hao na hivyo, kuamua kuwaachia.
Alisema pia ushahidi uliotolewa mashahidi wa Jamuhuri wameshindwa kuthibitisha kosa pasi kuacha shaka
"Tumeipitia hukumu yote sisi kama waendesha mashtaka wa TAWA na mawakili nguli wa Ofisi ya Mkurugenzi wa mashitaka hatujaridhika na uamuzi ndio sababu tumeamua kukata rufaa, na tayari tumeomba kupewa mwenendo wa kesi"amesema.
Amesema hata hivyo, licha ya kuwasilisha notisi ya kukata rufaa bado hawajapatiwa mwenendo wa shauri hilo, tangu mwezi Novemba. Hivyo tunaendelea kusubiria
Amesema kumekuwepo na changamoto katika kesi kadhaa ya ujangili hususan kesi zinazohisu meno ya tembo mkoani Manyara.
No comments:
Post a Comment