Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Dk. Selemani Jafo, akizungumza mbele ya Kamati ya kudumu ya Bunge ya maji na Mazingira, jijini Dodoma. |
Mwandishi Wetu, Dodoma
maipacarusha20@gmail.com
Serikali imeanza kuandaa Kanuni za Kutangaza na Kusimamia Maeneo 77 Nyeti na Lindwa yaliyoainishwa, inayotarajiwa kukamilika kabla ya Juni, 2024, ikiwa pia katika hatua ya kupunguza mgongano wa matumizi ya rasilimali kati ya wanyamapori na wananchi.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Dk. Selemani Jafo amebainisha hayo mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira jijini Dodoma hivi karibuni.
Amesema Serikali imeyapa kipaumbele maeneo 12 kwa ajili ya kufanyiwa tathmini zaidi kwa kuzingatia umuhimu wake kiikolojia kutokana na uharibifu wa mazingira.
“Tupo katika hatua za kupunguza mgongano wa matumizi ya rasilimali kati ya wanyamapori na wananchi, kupunguza mgongano wa matumizi ya rasilimali kati ya wanyamapori, uharibifu wa misitu unaotokana na shughuli za kibinadamu kama vile ukataji miti kwa ajili ya mkaa na kuni na uchimbaji holela wa madini,” amesema Waziri Jafo.
Akiwasilisha taarifa ya Hali ya Usimamizi wa Utekelezaji wa Mipango ya Ulinzi wa Mazingira katika maeneo Lindwa na Nyeti, Jafo amesema amesema maeneo yaliyo kwenye mpango huo ni yaliyoko kwenye madakio ya mito, maziwa, shoroba, milima na ardhi oevu
Ameyataja maeneo hayo kuwa ni Dakio la Mto Kihansi, Ziwa Challa lililoko Wilayani Rombo Mkoa wa Kilimanjaro, Mlima Livingstone na safu ya milima ya Mbeya katika mikoa ya Mbeya, Njombe na Ruvuma na safu ya Milima ya Makonde (Makonde Plateau Mountain Ranges).
Kwa mujibu wa Jafo, mengine ni maeneo nyeti na lindwa pendekezwa ambayo ni Mlima Mukendo mjini Musoma mkoani Mara, Ziwa Singidani, Ziwa Kindai na Ziwa Munang yaliyoko mkoani Singida na Ziwa Burunge, mifumo ikolojia ya hifadhi ya Tarangire na Ziwa Manyara yaliyoko mkoani Manyara.
Waziri Jafo amebainisha kuwa faida za kuwa na maneo lindwa na nyeti ni kuimarisha uhifadhi wa mifumo ikolojia yenye misitu, vyanzo vya maji na wanyamapori iliyopo nje ya maeneo yanayosimamiwa na sheria nyingine.
Amesema hatua hiyo itasaidia pia faida nyingine kulinda mazalia, makazi na malisho ya viumbe pia kuwakinga na madhara yatokanayo na majanga ya asili yanayoweza kutokea katika maeneo husika kama maporomoko ya ardhi, mafuriko na uvamizi wa wanyamapori.
No comments:
Post a Comment