WAZIRI KAIRUKI:SHIRIKIANANE NA WADAU WA UTALII KUBUNI NA KUTANGAZA UTALII NCHINI - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Saturday 24 February 2024

WAZIRI KAIRUKI:SHIRIKIANANE NA WADAU WA UTALII KUBUNI NA KUTANGAZA UTALII NCHINI

 




Na Lilian Kasenene,Same


maipacarusha20@gmail.com


Waziri wa Maliasili na Utalii Angella Kairuki amewaagiza wakuu wa mikoa, Wilaya na wakurugenzi kushirikiana na wadau wa utalli katika kubuni matukio ya  kuhamasisha na kutangaza utalii.


Waziri Kairuki amesema hayo  Wilayani Same mkoani Kilimanjaro wakati wa uzinduzi wa tamasha la kwanza la utalii liitwalo 'Same utalii Festival'. 


Amesema ilani ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2020 hadi 2025 katika ibara ya 67, Serikali imeelekezwa ifikapo mwaka 2025  idadi ya watalii iwe imeongezeka kufikia watalii milioni 5, wanaokuja kutembeleza hifadhi na maeneo mbalimbali ya utalii, watakaoingiza fedha zisizopungua dola za Kimarekani bilioni 6.


Amewataka kudumisha mila na desturi katika kutangaza utaliii ikiwemo kutumia ngoma, vyakula vya asili na dawa za asili ili kuwavutia zaidi watalii.


Hata hiyo amesema katika kipindi cha mwaka 2023 Januari hadi Novemba Tanzania imeweza kutembelewa na watalii milioni 1,808,205  ambapo alisema kwa mwaka 2024 watapiga hatua kubwa zaidi.


"Mwaka 2022 watalii walikuwa milioni 1,400,000, hivyo utaona ndani ya miezi 11 tumeweza kupata watalii takribani 400 ,000 wa ziada" amesema.


Kwa upande wake mkuu wa Wilaya ya Same Kasilda Mgeni amesema wazo la kuanzisha tamasha hilo ni kuibua maeneo yenye vivutio ambayo hayajatangazwa na ni matokeo ya ziara ya mafunzo waliyofanya baadhi ya wakuu wa Wilaya Nchini China, ambapo pamoja na mambo mengine walijifunza uzoefu wa kinacho fanyika nchini humo kuibua vyanzo vya mapato.


“Tulienda kwenye mafunzo Nchini China kujifunza mambo mbalimbali ya maendeleo na kujionea wanavyo fanya wenzetu kujiletea maendeleo ambapo nikiwa kule kuna sehemu tulipita tukaona mlima unaofanana kabisa na Mlima Kidenge uliopo kwenye wilaya yetu ya Same tofauti yake Mlima ule ulikua wa Kutengeneza na huu wa kwetu ni mlima asilia hivyo nikaona nikirudi jambo la kwanza ni kuangalia uwezekano wa kugeuza mlima huu kuwa furs,"amesema mkuu wa Wilaya ya Same Kasilda.


Amesema malengo ya tamasha hilo la Same Utalii Festival ni kuibua vivutio ambavyo havijatangazwa viweze kufahamika, kuviendeleza viweze kuwa sehemu ya mapato kwa kuwezesha watalii wakiwemo wazawa na raia wa kigeni kutembelea maeneo hayo ambayo katika wilaya ya Same pekee yapo mengi.


Mmoja wa mwananchi aliyeshiriki  kupanda mlima huo Adam Msuya amesema ni vema kukafanyika utafiti utakao shirikisha wakazi kwenye kila eneo kuainisha vivutio vilivyopo kwenye meneo yao ikizingatiwa mkazo kwenye kuhamasisha watalii unaelekezwa zaidi kwenye maeneo ambayo tayari yanafahamika.



No comments: