CHOMOKA AWA NAIBU MEYA MANISPAA MOROGORO,AELEZA KUFUATA MIONGOZO,KANUNI NA TARATIBU - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Friday 16 August 2024

CHOMOKA AWA NAIBU MEYA MANISPAA MOROGORO,AELEZA KUFUATA MIONGOZO,KANUNI NA TARATIBU

 

Naibu meya mpya Manispaa ya Morogoro Self Zahoro Chomoka



Na Lilian Kasenene, Morogoro 


maipacarusha20@gmail.com


KIKAO cha Mwaka cha Baraza la madiwani wa Manispaa ya Morogoro kimempitisha Seif Zahoro Chomoka kuwa naibu Meya wa manispaa hiyo ambapo amesema yeye hajachaguliwa kwa nia ya kuharibu miongozo, taratibu ama kanuni zilizopo, bali atafanyakazi na watu wote akimsaidia Meya wake


Naibu meya mpya ataongoza katika kipindi cha Mwaka mmoja.


Chomoka alipitishwa na kuapishwa baada ya Chama Cha mapinduzi CCM kupeleka jina lake na kufanya kuwa mgombea pekee.


Akizungumza baada ya kuapishwa, Chomoka alisema kuwa yupo tayari kumsaidia kazi mstahiki meya, hivyo aliomba kupewa ushirikiano na madiwani wenzake pamoja na watendaji wakiwemo wakuu wa Idara ili kuwezesha upatikanaji  maendeleo ya wananchi.


Aidha Chomoka alishauri kuwa suala kubwa na lililo na umuhimu kwao ni kushirikisha mamlaka nyingine kwenye kufanya maamuzi yanayohusu mstakabali wa maendeleo ya Manispaa  hiyo ya Morogoro.


“Naomba Tusijifungie chumbani peke yetu na tukatoka na maamuzi yetu sisi wenyewe kwani tunapoyapeleka mbele wakati mwingine tunakwama na ukifuatilia kwa ndani kwa nini tumekwama  utakutana na taarifa ya kwamba maamuzi yetu hayakuwa shirikishi,” alisema Naibu meya Chomoka.


Meya wa Manispaa hiyo Pascal Kihanga kwenye taarifa yake ya utendaji na uwajibikaji wa Manispaa hiyo katika mwaka wa fedha 2023/2024 iliyowasilishwa kwenye mkutano wa mwaka wa Baraza la Madiwani alisema dhamila ya kuwa Jiji bado wanayo.


Kihanga pia alisema ujio wa reli ya mwendo Kasi utawafanya Manispaa kuwa na wawekezaji wengi na idadi ya watu kuongezeka.


Akizungumzia suala ya usafi wa mji wa Morogoro aliwataka madiwani kuona wajibu na kujitathimini huku akiwataka kwenye maeneo ya kuhimiza suala la usafi na maeneo kusafishwa.


Pia aliwataka kutumia Lugha zenye staha kwa watendaji wa kata kwani ndio wasaidizi wao wakubwa.


Jackline Msumba kutoka sekretarieti ya mkoa wa Morogoro akizungumza kwa niaba ya kamishana wa maadili alipongeza uwepo wa uadilifu na maadili kwa watumishi na kwamba wako vizuri.


"Lazima tutambue kwamba bado kuna kazi ya kufanya kama viongozi  mnawajibika kusimamia uadilifu kwa walio chini yenu tusiache kusimamia uadilifu kwenye Idara na vitengo vyetu,"alisema Msumba.


Mwisho.

No comments: