JOWUTA, OSHA KUSHIRIKIANA USALAMA WA AFYA KWA WANAHABARI KAZINI - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Friday 16 August 2024

JOWUTA, OSHA KUSHIRIKIANA USALAMA WA AFYA KWA WANAHABARI KAZINI


Viongozi wa JOWUTA na OSHA katika picha ya pamoja 



Mtendaji Mkuu wa OSHA, Hadija Mwenda 




Na Mwandishi Wetu, DSM

maipacarusha20@gmail.com 


Wakala wa Usalama wa Afya Mahala pa Kazi (OSHA) umesema kuwa utashirikiana na Chama cha Wafanyakazi wa Vyombo vya Habari Tanzania (JOWUTA) kuhakikisha elimu ya masuala ya usalama wa afya mahala pa kazi inawafikia wafanyakazi na jamii kwa ujumla.

Hayo yamebainishwa leo jijini Dar es Salaam na Mtendaji Mkuu wa OSHA, Hadija Mwenda wakati akifungua mafunzo ya siku moja kwa waandishi wa habari yenye lengo la kujengea uelewa kuhusu usalama mahala pa kazi.

Mafunzo hayo yametolewa na OSHA kwa waandishi hao wa habari zaidi ya 50 kutoka Dar es Salaam na Pwani ambao ni wanachama wa JOWUTA.

Akizungumza na waandishi hao, Mwenda amesema katika tathmini waliyoifanya wamegundua kuwa kuna uelewa mdogo kwa wadau juu ya kazi zinazofanywa na Osha na kwamba ili kukuza uelewa huo wanapaswa kushirikiana na waandishi wa habari.


Amesema wamejipanga kuhakikisha elimu ya masuala ya afya mahala pa kazi inatolewa kwa kundi hilo kwani wanaamini kupitia waandishi wa habari itawafikia wananchi hasa wafanyakazi na wataelewa kwa undani zaidi juu ya usalama wa afya zao mahala pa kazi.


“Waandishi wa habari ni kundi muhimu na ndio macho na masikio ya wananchi, ili liendelee kupata taarifa nzuri lazima liwe salama ndio maana tukasema jukumu letu tuwapatie elimu na wao waitoe hiyo elimu kwa jamii,” amesema





Mwenda amesema kupitia waandishi wa habari jamii itapata kuelewa kwa nini kuna sheria ya usalama mahala pa kazi na kusisitiza wanahabari wanaendelea kuwa nguvu kazi yenye afya inayofanya kazi kwa usalama.

“Tumetoa mafunzo haya ili waandishi wa habari nao wavitambue vihatarishi kwa sababu hakuna mazingira ya kazi ambayo hayana vihatarishi, kazi yetu sisi OSHA ni kuhakikisha vihatarishi hivyo havimuathiri mfanyakazi ili aweze kufanya kazi kwa tija hata akistaafu basi astaafu akiwa na afya njema,” amesema

Mwenyekiti wa JOWUTA, Mussa Juma akizungumza na waandishi wa habari 


Aidha amesema OSHA inapofanya ukaguzi mahala pa kazi inataka kuangalia namna ambavyo watu wanafanya kazi katika mazingira yanayotakiwa kwa mujibu wa sheria.

Naye Mwenyekiti wa JOWUTA, Mussa Juma amesema wanatambua kuwa waandishi wa habari wanakabiliwa na changamoto nyingi katika maeneo yao ya kazi hivyo mafunzo hayo yatawafanya kupata uelewa na kuwa mabalozi wazuri.

“Tunatambua kuwa mafunzo haya ni muhimu kwa waandishi wa habari na tunaimani kuwa ushirikiano huu tuliouanzisha na OSHA utadumu na tutaweza kuwafikia waandishi wa habari wengi zaidi nchini,” amesema

Mussa Juma  amewaomba OSHA kushirikiana na JOWUTA kutoa elimu kwa wanachama wa JOWUTA nchi nzima ambao ni zaidi ya 400 na OSHA imekubali kushirikiana nao.

Aidha wameomba OSHA isaidie kufanya ukaguzi mara kwa mara katika vyombo vya habari ili kuwahakikishia wanahabari Usalama mahala pa kazi, pia kusaidia Wamiliki wa vyombo vya habari vya binafsi na Umma wawe na sera  za Usalama na afya mahala pa kazi.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa JOWUTA, Suleiman Msuya amesema chama hicho kinafanya kazi kwa mujibu wa Sheria na kwa sasa kina jumla ya wanachama 400 nchi nzima na kwamba maombi yao kwa OSHA ni kuendelea kutoa mafunzo hayo kwa wanachama wao wengine waliopo mikoani.

“Dar es Salaam tuna wanachama zaidi ya 80 lakini tuliona katika mafunzo hayo tuwe na washiriki 50 kutoka Dar es Salam na Pwani.

Tunaamini mafunzo haya ni muhimu kwa waaandishi kupitia elimu watakaoipata watakuwa mabalozi wazuri kwa jamii hasa kutangaza kazi zinazofanywa na OSHA.“Tunawashukuru OSHA kwa kutoa mafunzo haya, tunawaomba mkienda kufanya operesheni zenu tushirikisheni ili umma utambue mnachokifanya,”amesema Msuya.

No comments: