DC KILOMBERO AIPA KONGOLE REA - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Sunday 4 August 2024

DC KILOMBERO AIPA KONGOLE REA

 

MKUU wa Wilaya ya Kilombero Dunstan Kyoba akizungumza na Viongozi wa REA

MKUU wa Wilaya ya Kilombero Dunstan Kyoba akizungumza na Viongozi wa REA 


Na Lilian Kasenene, Morogoro


maipacarusha20@gmail.com


MKUU wa Wilaya ya Kilombero Dunstan Kyoba amesema Kituo cha kupoza umeme cha Ifakara ni kituo  mkombozi kwa Wilaya za Ulanga na Kilombero pamoja na vijiji vyake vyote.


Aliyasema hayo alipotembelewa na Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) wilayani Kilombero walipokuwa wakijadili ziara ya Rais Samia Suluhu Hassan Mkoani Morogoro ambapo atafanya ziara siku ya jumapili tarehe 4 Agosti,2024 katika kituo cha kupozea umeme kilichojengwa na REA kwa ufadhili wa umoja wa Ulaya pamoja na Serikali ya Tanzania.


"Kituo hiki cha kupozea umeme ni cha kisasa na tangu kianze kufanya kazi kimeendelea kuchochea ukuaji wa uchumi katika Wilaya za Kilombero, Ulanga na Malinyi," alisema Kyoba.


Alifafanua kuwa umeme wa uhakika unahitajika katika uendeshaji viwanda vya uchimbaji wa madini aina ya graphite katika wilaya ya Ulanga na uongezaji thamani mazao ya chakula hususan mahindi na mpunga.


Alipongeza REA kwa kupunguza kero za upatikanaji umeme katika sekta ya afya wilayani Kilombero hususani katika hospitali ya St.Francis na Good Samaritan mjini Ifakara.


"Wilaya ya Kilombero ni Wilaya ya Uhifadhi hivyo kituo hiki cha kupozea umeme kimepunguza kasi ya ukataji miti hovyo na hivyo kupungua kwa kiasi kikubwa cha uharibifu wa misitu," amesema Mhe.Kyoba


Aidha, aliisisitiza REA kuhakikisha inaendelea kutoa elimu kwa umma kuhusiana na masuala mazima ya nishatisafi ya kupikia pamoja na ugawaji wa mitungii ya gesi kwa  wananchi wa Wilaya ya kilombero na vijiji vyake kwani. 


"Kilombero imefunguka matumizi ya gesi ya kupikia yataongezeka ikiwemo matumizi mazima ya nishati mbadala na majiko ya banifu, tuendelee kuhamasisha wananchi,"alisisitiza.


Naye Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA),Hassan Said alisema miradi ya REA imetawanyika nchi nzima  hivyo nia kubwa ya Wakala ni kuhakikisha kuwa vijiji vyote nchini kufikia Desemba 2024 vinakuwa na umeme. 


"Maisha ya watanzania waishio vijijini watatumia umeme huu sio kuwashia taa tu bali kubadilisha maisha yao kiuchumi kwa kuwa na shughuli mbalimbali za kuwaingizia kipato," alisema Mhandisi Said.


Wakala wa Nishati Vijijini REA,ulianzishwa kwa malengo kuwezesha upatikanaji wa nishatisafi vijijini.


Mwisho..

No comments: