WAKAMATWA NA VIPANDE 29 VYA MENO YA TEMBO MOROGORO - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Sunday 18 August 2024

WAKAMATWA NA VIPANDE 29 VYA MENO YA TEMBO MOROGORO

 


Kamanda wa polisi mkoa wa Morogoro Alex Mkama



Na Lilian Kasenene,Morogoro


maipacarusha20@gmail.com


WATU wanne wanaodaiwa kukutwa na nyara za serikali vipande 29 vya Meno ya Tembo wanashikiliwa na Jeshi la Polisi mkoani Mirogoro.


Watu hao wanadaiwa kukamatwa katika wilaya ya Kilosa na Morogoro.


akizungumza na Waandishi wa Habari, Kamanda wa polisi mkoa wa Morogoro Alex Mkama alisema oparesheni iliyofanywa kwa kipindi cha  mwezi mmoja na Jeshi hilo ilifanikiwa kukamatwa kwa  wahalifu hao na wengine kwenye matukio mbalimbali.


"Mafanikio yamepatikana katika kuwafuatilia majangili na wawindaji haramu wa wanyama pori kwenye hifadhi zetu kwa kipindi cha  mwezi mmoja na kuwakamata watuhumiwa "alisema.


Mkama aliwataja waliokamatwa kuwa ni Yahaya Bakari (60) mkulima mkazi wa Chalinze, Masima Mlugu Ntumbi mkulima mkazi wa Mlenge vianzi, Juma Ramadhani Zinga (46) mkulima mkazi wa Bagamoyo na Mansour Juma Abdallah (40)  mkulima mkazi wa Dar-es-salaam.


Aidha katika  tukio lingine kamanda Mkama alisema Polisi  imewakamata watuhumiwa saba (7) ambao walipanga na kushiriki kufanya utapeli kwenye nyumba ya watawa wa kike huko eneo la Bigwa (Bigwa sisters).


Alisema tukio hilo limetokea Agosti 16, 2024 eneo la Bigwa, manispaa ya Morogoro ambapo watuhumiwa waliingia kwa jinai ndani ya eneo la makazi ya watawa na kunadi madini bandia kwa  ajili ya kujipatia kipato na walijitambulisha kuwa watafiti wa mali kale na kwamba eneo hilo ni sehemu ya utafiti wao.


Alisema watuhumiwa walikamatwa wakiwa na simu 13, laini za simu 27 za mitandao mbalimbali ya simu yenye usajiri wa majina tofauti tofauti ambazo huzitumia kwa utapeli.


Aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Janeth Winston Mhuvile (53) mfanyabiashara mkazi wa Kigurunyembe, Samson Amos Can (51) mkulima mkazi wa  Uhuiko Songea, Ramadhani Nassor (33) mfanyabiashara mkazi wa Dar-es-salaam, Karimu Mlawa (43) mfanyabiashara mkazi wa Dar-es-salaam, Daniel David (40)  mfanyabiashara mkazi wa Dar-es-salaam, Rongido Myovela (66) mfanyabiashara mkazi wa Dar-es-salaam, Joakim Mwinyimvua (65) mfanyabiashara mkazi wa Kilimanjaro.


Aidha, alisema  Mussa Emmanuel Nongolo (44) alikamatwa baada ya kujiwasilisha kuwa ni mtumishi wa serikali,  na alijitambulisha hivyo kwa lengo la kutaka kujipatia kipato kwa watu aliowakusudia.


Pia  Jeshi la Polisi limefanikiwa kumkamata Robert Amandus (45), mkazi wa kidatu aliyekuwa anatafutwa kwa muda mrefu baada ya kumuua Ekonia Simon (30) tukio ambalo lilitokea Februari 16, 2024 ambapo mtuhumiwa na mwenzake anayetafutwa walimuua kwa kumkata na kitu chenye makali sehemu mbalimbali za mwili wake.


Vilevile  Selemani Mohamedi (34) mkazi wa Mafisa alikamatwa na Jeshi la Polisi huko Mlali Wilaya ya Mvomero baada ya kukutwa yeye na wenzake 14 ambao walitoroka wakiwa wanawafanyia upekuzi majumbani kwa wananchi mbalimbali wakijitambulisha kuwa ni askari polisi wanaofanya msako wa bangi ambapoo wananchi walishituka na kutoa taarifa ambapo polisi walifika na kufanikiwa kuzima jaribio la utapeli. 


Mwisho.

No comments: