VIJANA MANYARA WATAKIWA KUVUNJA UKIMYA DHIDI YA UKATILI WA JINSIA - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Sunday 29 September 2024

VIJANA MANYARA WATAKIWA KUVUNJA UKIMYA DHIDI YA UKATILI WA JINSIA

 





Na Epifania Magingo, Manyara 


maipacarusha20@gmail.com 


Vijana wametakiwa kuvunja ukimya huku wakipaswa kuzungumza pale ambapo wanapitia changamoto mbalimbali za ukatili ili waweze kupata msaada wa haraka wa kimatibabu na  kisheria kwa kuwachukulia hatua waliohusika na ukatili huo na taarifa zao zitatunzwa kwa siri kama yanavyoelekeza maadili ya kazi.


Hayo yameelezwa na Afisa Maendeleo ya Jamii na Mratibu wa kutekeleza mpango kazi wa Taifa wa kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto Mkoani Manyara Anna Fisoo wakati akizungumza na wanafunzi kwenye uzinduzi wa kampeni ya “tuwaambie kabla hawajaharibiwa” inayosimamiwa na Jeshi la Polisi upande wa Dawati la Jinsia Mkoa wa Manyara.


Katika uzinduzi huo Afisa Maendeleo Anna Fisoo amesisitiza vijana kutoa taarifa kwasababu bado kunachangamoto ya matukio mengi ya ukatili ambayo yanasuluhishwa kifamilia jambo ambalo linawafanya washindwe kupatiwa haki zao za msingi kama sheria zinavyoelekeza.


“Kunachangamoto ya watu kumalizana  kimila, unapigwa halafu wazee wanakuja wanamalizana wanakula mbuzi, au mtoto ametiwa mimba wazee wanamalizana na hawafikirii ndoto za yule mtoto, hivyo naomba wanafunzi vunjeni ukimya kama kuna kitu ambacho kinakutesa ni vyema ukazungumza ili uwe huru na ukatibiwe na taarifa zako zinabaki kuwa siri”.


Aidha, Anna Fisoo amelishukuru Jeshi la Polisi kitengo Cha Dawati la Jinsia Mkoa wa Manyara kwa kuendelea kutoa ushirikiano na kusimamia vyema kesi zinazoripotiwa na hukumu kutolewa kama sheria zinavyoelekeza ili iendelee kuwa fundisho kwa wengine.


Kampeni ya “tuwaambie kabla hawajaharibiwa” ni kampeni yenye lengo la kutoa elimu kuhusu ukatili kwa watoto na vijana nchi nzima ili wajue namna kuepuka changamoto hizo na wapi pakutolea taarifa pale ambapo mtoto au kijana anakumbwa na changamoto ya aina yeyote ya ukatili.


Takwimu zilizotolewa kwenye mfumo wa Afya wa kutolea taarifa zinaeleza Januari mpaka mpaka Agasti 2024,takribani matukio 6261 ya ukatili dhidi ya wanawake na watoto yameripotiwa ambapo kwa mwaka 2023 matukio 8360 yalitipotiwa.

No comments: