Halmashauri Tunduru yafafanua madai wagonjwa kubebwa kwa tenga - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Sunday 29 September 2024

Halmashauri Tunduru yafafanua madai wagonjwa kubebwa kwa tenga

 

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru, Chiza Marando

🔩🔩Baada ya taarifa ya wagonjwa kubebwa kwenye tenga katika Kata ya Mchoteka wilayani Tunduru, Halmashauri ya Wilaya hiyo imefafanua uhalisia wake.


Na mwandishi wetu,Ruvuma

maipacarusha20@gmail.com


Tunduru. Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru, Chiza Marando amesema taarifa zilizosambazwa kuhusu changamoto ya upatikanaji wa gari la kubebea wagonjwa katika Kata ya Mchoteka imezushwa.


Marando alisema uhalisia, eneo hilo na maeneo mengine ya Halmashauri hiyo ya Tunduru, hayana changamoto ya gari la kubebea wagonjwa kwa kuwa Serikali ilikabidhi magari manne kwa ajili ya shughuli hiyo.


Taarifa ya halmashauri hiyo, inajibu picha zilizosambaa katika mitandao ya kijamii zikionyesha mgonjwa akiwa amebebwa kwenye tenga kupelekwa hospitali.


Ambapo mkurugenzi huyo alifafanua kuhusu taarifa hiyo na alisema kuna jumla ya magari manne ya kubebea wagonjwa kwenye zahanati na vituo vya afya.


Alisema yamewekwa katika Tarafa kwa kuzingatia urahisi wa uratibu wa rufaa zote.


“Gari la kubebea wagonjwa katika Tarafa ya Nalasi lipo katika kituo cha Afya Nalasi,Gari hii hubeba wagonjwa katika kata zote za Tarafa ya Nalasi ikiwemo Kata ya Mchoteka na Kituo cha Afya Mchoteka,” alisema.


Sambamba na hilo, alisema kupitia mpango wa M-mama halmashauri hiyo ina jumla ya madereva ngazi ya jamii 20 waliopo katika Kata zote ikiwemo Mchoteka.


Alisema madereva hao hutumika kusafirisha kina mama na watoto wachanga wakati wa dharura.


“Niendelee kusisitiza kuwa taarifa zinazoendelea kusambazwa katika mitandao ya kijamii zipuuzwe kwani hazina uhalisia na zina lengo la kuichafua Serikali,” alisema.


Amewasisitiza wananchi waendelee kupata na kutumia taarifa sahihi kutoka katika vyanzo na mamlaka halali zinazotambulika.


Katika siku za hivi karibuni kumekuwa kukisambaa Picha ikionyesha wagonjwa kubebwa na Tenga kupelekwa kituo cha afya kata ya Mchoteka.


Mwisho.

No comments: